Februari 24,2022 Alhamisi: Juma La 7 La Mwaka

SOMO 1: Yak. 5: 1-6
Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.

Wimbo Wa Katikati Zab. 49: 13-19

 1. Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao
  Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao.
  Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu,
  Na mauti itawachunga;
  Watu wanyofu watawamiliki asubuhi.
  K: Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
 2. Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu.
  Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu,
  Atanitoa mkononi mwa kuzimu,
  Maana atanikaribisha. (K)
 3. Usiogope mtu atakapopata utajiri,
  Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
  Maana atakapokufa hatachukua chochote;
  Utukufu wake hautashuka ukimfuata. (K)
 4. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai,
  Na watu watakusifu ukijitendea mema,
  Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake;
  Hawaona nuru hata milele. (K)

INJILI: Mk. 9:41-50
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia: Hatakosa thawabu yake. “Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.”

TAFAKARI
HAKI WAKATI WOTE ITAJIDHIHIRISHA: Kila mmoja wetu hujishughulisha na kazi fulani angali hapa duniani lengo hasa ni kujipatia riziki za maisha. Wapo wanaopitiliza na hivyo kuwa na roho ya kujilimbikizia mali hadi kunyonya na kuonea wengine na hata kukosa utu. Wanawatumikisha wengine kazi kama punda. Usishangae utakuta mtu anasimamia vibarua wanaovuna shambani mwake. Wakati wao wanapigwa jua na kazi ngumu, yeye yuko tu kajifungia kwenye gari akipiga simu tu na ikifika jioni baada ya kazi malipo wanayopata hayalingani na kazi waliyofanya. Lakini kwa vile wao ni wahitaji hawana namna inabidi wakubaliane na hali. Yakobo leo anatushtua tuwe makini, tusiwanyanyase wanyonge. Hata Kristo katika Injili anagusia uzuri wa kumjali mwingine, “Yeyote atakayewanywesha kikombe cha maji….”. Tunaalikwa tuwe na utu. Tujue maisha yajayo yanatutaka tusaidiane.

SALA: Tusali kumwomba Mungu atujalie moyo wa kuwajali wengine.