Februari 23,2022; Jumatano: Juma La 7 La Mwaka

Mt. Polikarpo, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani

SOMO 1: Yak. 4: 13-17
Haya basi, ninyi msemao, leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya. Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.
Wimbo Wa Katikati Zab. 49:1-2, 5-10

 1. Sikieni haya, enyi mataifa yote;
  Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani.
  Watu wakuu na watu wadogo wote pia,
  Tajiri na maskini wote pamoja.
  K: Heri walio maskini wa roho,
  maana ufalme wa mbinguni ni wao.
 2. Kwa nini niogope siku za uovu,
  Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
  Wa hao wanaozitumainia mali zao,
  Na kujisifia wingi wa utajiri wao. (K)
 3. Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu,
  Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
  Maana fidia ya nafsi zao ina gharama,
  Wala hana budi kuiacha hata milele
  Ili aishi sikuzote asilione kaburi. (K)
 4. Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa;
  Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja,
  Na kuwaachia wengine mali zao. (K)

INJILI: Mk. 9:38-40
Yohane alimjibu Yesu akamwambia, “Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.” Yesu akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.”

TAFAKARI
UJASIRI HUMFANYA MTU KUWA IMARA KIIMANI: Kanisa leo linaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Polikarpo Askofu na shahidi. Katika maisha yake tunaelezwa kuwa alikuwa jasiri bila woga na kutetea imani yake mpaka mwisho. Wengi wetu tukitikiswa kidogo tu tunayumba. Leo hii tunashuhudia dini na madhehebu mbalimbali kila kona yanaibuka, wanaohamia huko ni Wakristo Wakatoliki wenzetu waliobatizwa na kupewa Kipaimara. Ukimuuliza kwa nini anajibu, ‘Nimeokoka’. Je ina maana katika ukatoliki hakuna wokovu? Tumekuwa na imani vuguvugu, ndio hiyo Yakobo anasema, “Mvuke uonekanao kwa kitambo kisha hutoweka.” Tumeshindwa kuwa imara na hata mitume wa Yesu walikuwa na wasiwasi hadi kuwakataza waliokuwa wanajitahidi katika imani yao.

SALA: Yesu Mwema, tunaomba uimarishe imani yetu.