Februari 22,2022; Jumanne: Juma La 7 La Mwaka

Ukulu Wa Mt. Petro, Mtume
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: 1 Pet. 5:1-4
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 23

 1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
  Sitapungukiwa na kitu.
  Kitika malisho ya majani mabichi hunilaza,
  Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
  K: Bwana ndiye Mchugaji wangu,
  sitapungukiwa na kitu.
 2. Hunihuisha nafsi yangu, na kuniongoza,
  Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
  Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
  Sitaogopa mabaya,
  Kwa maana wewe upo pamoja nami,
  Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
 3. Waandaa meza mbele ya macho yangu,
  Machoni pa watesi wangu.
  Umenipaka mafuta kichwani pangu
  Na kikombe changu kinafurika. (K)
 4. Hakika wema na fadhili zitanifuata,
  Siku zote za maisha yangu,
  nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

INJILI: Mt. 16:13-19
Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, “Watu hunena Mwana wa adamu kuwa ni nani?” Wakasema, “Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.” Akawaambia, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Simoni Petro akajibu akasema, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu akajibu, akamwambia, “Heri wewe Simoni Bar-yona kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”

TAFAKARI
HESHIMA HULETA UTULIVU KATIKA JAMII: Kanisa leo linaadhimisha sikukuu ya ‘ukulu wa Mtakatifu Petro’. Sikukuu hii ujumbe wake hasa ni kuhusu mamlaka ya Baba Mtakatifu. Kanisa Katoliki lina mfumo rasmi wa uongozi kuanzia Baba Mtakatifu hadi mkristo mwamini katika JNNK. Kila kiongozi anayo heshima yake ambayo kwayo ile neema ya Mungu itarajiwayo huweza kuonekana au kudhihirishwa. Katika makabila mengi kuna vitu wanavipa heshima fulani kutokana na umuhimu wake na hasa wa kufanya ile jamii ikae kwa uelewano. Wengine wanaheshimu miti mikubwa na unakuta mtu haruhusiwi kuukata, na unapoukata kuna sadaka fulani ambayo hutolewa hapo. Vivyo hivyo nasi kwa imani yetu, tunatoa heshima kwa kiti alichokabidhiwa Petro, tukilenga kuheshimu yale mamlaka aliyopewa, tukiamini anatuchunga vyema kama somo la kwanza linavyotueleza. Na Injili imekazia hilo, mitume wengine waliheshimu hilo na ndio maana walimwacha Petro ajibu kwa niaba yao.

SALA: Mungu Mwenyezi, tunamwombea Baba Mtakatifu na Mahalifa wake ili watuongoze vyema. Baba yetu….Salamu Maria….Atukuzwe Baba……