Mt. Petro Damiano Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yak. 3: 13-18
N’nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima. Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 19: 7-10
- Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini
Humtia mjinga hekima.
K: Maagizo ya Bwana, huufurahisha moyo. - Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia mamco nuru. (K) - Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K) - Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali. (K)
INJILI: Mk. 9:14-29
Yesu na Petro na Yakobo na Yohane walipowafikia wanafunzi, waliona mkutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao; mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu. Akawauliza, “Mnajadiliana nini nao?” Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze.” Akawajibu, akasema, “Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.”
Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaaanguka chini; akagaagaa, akitokwa na povu. Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto. Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu. Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua; naye akasimama. Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba.
TAFAKARI
NIJAZE HEKIMA YA KUFAHAMU NINAYOFAA KUTENDA: Nukuu hili tunalipata katika masomo ya leo. Katika somo la kwanza tunaona umuhimu wa hekima. Swala kuu ni, ‘Ni nani aliye na hekima na ufahamu wa kweli?’ Ili kuyatenda matendo yanayostahili, inatupasa tuwe wenye hekima. Hekima ni kielelezo mwafaka katika maisha yetu na katika matendo yetu. Bila hekima, changamoto hutusonga na mwishowe tunakosa njia timilifu ya kujinasua kutoka kwa yale yanayotusonga. Katika injili tunamwona Yesu anawauliza wanafunzi wake, “Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini?” Yesu anasema haya baada ya kutambua kwamba wanafunzi wake wameshindwa kumtoa pepo aliye ndani ya kijana aliyeletwa kwao. Hawana fahamu ya wanachopaswa kutenda ili kumsaidia kijana huyo. Mwishowe, Yesu anawaeleza njia inayatumika kutoa pepo sio kwa neno tu bali kwa kuomba. Kutokana na tukio hili, inatupasa tuwe na hamu ya kuwa na hekima ili tusiwe wale wasioelewa wanachofaa kutenda. Hekima ya kweli sharti iandamane na sala na ucha Mungu.
SALA: Yesu, tujaze hekima ili tupate maarifa yatakayotuwezesha kutenda kulingana na unayoamuru.