Februari 20, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 7 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO LA I: 1Sam. 26: 2, 7-9, 12-13, 22-23
Sauli aliondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, “Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa ilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyoosha mkono wake juu ya masihi wa Bwana, naye akawa hana hatia?” Basi Daudi akalitwaa lile fumo na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa Bwana umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng’ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao. Daudi akapiga kelele akasema, “Litazame fumo hili, Ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae. Naye Bwana atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake; maana Bwana amekutia mikononi mwangu leo, nami nalikataa kuunyoosha mkono wangu juu ya masihi wa Bwana.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 103 1-4,8,10, 12-13

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
  Naam, vyote vilivyo ndani yangu
  Vilihimidi jina lake takatifu.
  Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K) Bwana amejaa huruma na neema

 1. Akusamehe maovu yako yote,
  Akuponya magonjwa yako yote,
  Aukomboa uhai wako na kaburi,
  Akutia taji la fadhili na rehema, (k)
 2. Bwana amejaa huruma na neema,
  Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
  Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
  Wala hakutulipa kadiri ya maovu yetu. (k)
 3. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
  Ndivyo alivyotuweka dhambi zetu mbali nasi.
  Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
  Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. (k)

SOMO 2: 1 Kor. 15: 45-49
Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo. Kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye mbinguni.

SHANGILIO Yn. 13 : 34
Aleluya, aleluya
Nawapa amri mpya, mpendane,
Kama vile nilivyowapenda ninyi,
Nanyi mpendane vivyo hivyo.
Aleluya.

INJILI: Lk. 6: 27-38
Siku ile Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Nawaambia ninyi mnaosikia, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikini wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigae shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyaye vitu vyako usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata mwenye dhambi huwapenda wale wampendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili wawarudishie vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma, msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa: kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

TAFAKARI
TUPENDANE TUWAPITE WASIOMJUA MUNGU: Jambo hili linasemwa na injili na kuungwa mkono na masomo mawili yaliyotangulia kusomwa. Mintarafu migogoro na kukoseana, Bwana wetu Yesu ameshauri tuiishi enzi ya tatu na ya pekee ya mambo. Enzi ya kwanza ilikuwa ya mfalme Hammurabi. Enzi ya pili ilikuwa ya torati. Mintarafu enzi ya kwanza, katika miaka ya 1750 K.K. alikuwapo mfalme Hammurabi ambaye aliamini kuhasimiana na kufanyiana maovu kungalikoma kwa kutoa adhabu kali kupita kile alichofanya aliyekosea. Sheria alizozitunga zilikuwa kali kweli kweli kiasi cha mtu alimuua mtu mmoja aliadhibiwa kwa kuuliwa ndugu na jamaa zake sabini. Enzi yake ilikuwa ilikuwa ni ya kulipana kisasi na kukong’otana kwenye kupindukia kosa.
Baada ya miaka 500, yaani katika miaka ya 1250 ikaingia enzi ya torati. Torati ilitaka kukabiliana na kuhasimiana na kufanyiana maovu kwa kumwadhibu mkosefu kwa kiasi kile kile alichomtendea mwingine. Ilikuwa enzi ya kufanyiana sawa kwa sawa. Kama mtu alimvunja mtu mkono na yeye alivunjwa mkono. Kama alimvunja jicho mtu na yeye alivunjwa jicho hivyo hivyo. Kama mtu alimvunja mguu mtu na yeye alivyunjwa mguu namna hiyo hiyo na kama alimuua mtu na yeye aliuawa. Ndiyo ilikuwa sheria ya mkono kwa mkono, jicho kwa jicho, mguu kwa mguu na uhai kwa uhai. Watu wa wakati wa torati walishusha pumzi wakiona haki inatendeka kwa sheria hiyo ya jino kwa jino.
Mwanzoni mwa karne ya kwanza B.K., Yesu Kristo akaleta enzi yake ya pekee. Yesu akafundisha kusameheana na siyo kukong’otana kwenye kupitiliza makosa wala kulipana kisasi sawa kwa sawa. Kwa maagizo yake ametaka wafuasi wake tupendane, tuhurumiane, tusameheana na tutendeane kiuadilifu tuwapite wasiomjua Mungu. Tuwashinde kwa wema wanaotunenea maneno mabaya, wanaotupiga,wanaotunyang’anya vyetu, wasiotupenda, wanaotukopa, wasio na shukrani, wasiotusalimu, wanaotuhukumu, wanaotudhulumu, wanaotaka kutuua na kadhalika. Hivyo ndivyo injili inavyotuasa. Inatolewa sababu ya sisi kutenda tofauti na wasiomjua Mungu, ndiyo jitihada za kujifananisha na Baba yetu. Mtoto wa mwadilifu yafaa awe mwadilifu, mtoto wa mkamilifu yafaa naye awe mkamilifu, mtoto afanane na baba au mama yake.
Somo la kwanza linatupa mfano wa kuwasamehe wanaotuwinda kusudi watuue. Kijana Daudi aliyekuwa akiwindwa na mfalme Sauli kusudi amuue, anamwachilia mfalme Sauli katika nafasi nzuri iliyojipa kuweza kumchinja. Anafahamu kuwa atakayewaua mpakwa wa Bwana, Bwana mwenyewe atawalipia kisasi.
Katika Somo la pili tunafananisha na Kristu kwakuzaliwa upya katika Utatu Mtakatifu (Baba, Mwana na Roho Mtakatifu). Tumepewa sura ya Adamu wa pili, Yesu Kristo. Kwa hiyo, hatuna budi kuenenda kwa namna mpya. Tufanane na Mungu Baba, tufanane na Yesu Kristo, tufanane na Roho Mtakatifu. Tukifanana na Nafsi hizi tatu za Mungu wetu, tutapendana na tutaenenda kuwapita wasiomjua Mungu. Kulipana kisasi hakutakuwa utamaduni wetu isipokuwa kusameheana na kuwapenda hata maadui wetu.

SALA: Ee Mungu, tusaidie tufanane nawe. Tuenende vyema tuwapite wasiokujua. Amina.