Februari 19, 2022; Jumamosi: Juma la 6 la Mwaka

SOMO I: Yak. 3:1-10
Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua kuwa tutapata hukumu kubwa zaidi.
Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili watutii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha. Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, wanafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka Baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.
Wimbo Wa Katikati Zab. 12: 2-3. 4-5. 7-8

 1. Bwana, uokoe, maana mcha Mungu amekoma,
  Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.
  Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe,
  Wenye midomo ya kujipendekeza;
  Husemezana kwa mioyo ya unafiki;

(K) Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi.

 1. Bwana ataikata midomo yote ya kujipendekeza,
  Nao ulimi unenao maneno ya kiburi;
  Waliosema, kwa ndimi zetu tutashinda;
  Midomo yetu ni yetu wenyewe,
  Ni nani aliye bwana juu yetu? (K)
 2. Maneno ya Bwana ni maneno safi,
  Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi;
  Iliyosafishwa mara saba.
  Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi,
  Utatulinda na kizazi hiki milele. (K)

INJILI: Mk 9: 2-13
Siku ile Yesu aliwatwaa Petro, na Yakobo, na Yohane, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimetameta, meupe mno jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu.
Petro akajibu, akamwambia “Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.” Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.” Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, huko kufufuka katika wafu maana yake nini?
Wakamwuliza, wakisema, “Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?” Akajibu akawaambia, “Ni kweli Eliya yuaja kwanza, na kurejeza upya yote; lakini pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa.”

TAFAKARI
MIILI YETU NI UDHIHIRISHO WA MUNGU: Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake. Kaipa miili yetu viungo mbalimbali na kila kimoja kina kazi yake na umuhimu wake. Kila kimoja tunaambiwa kipo kwa ajili ya kumsifu na kumdhihirisha Mungu. Yakobo katika somo la kwanza ameonyesha umakini unaotakiwa katika matumizi ya ulimi. Ulimi huu ndio unaotumika kutoa maneno ya baraka au balaa. Kuna watu wakiongea lazima viunganishi vya matusi viwepo. Huko ni kutumia vibaya kiungo hiki. Ulimwengu huu umefikia hapa kwa sababu ya ndimi zetu, magomvi yasiyokoma hadi vita. Hata katika Injili tunaona jinsi Musa na Eliya wanavyotumia vyema ndimi zao kwa kuzungumza na Yesu. Hili litupe funzo kuwa ulimi ukitumiwa vyema Mungu anajidhihirisha kwetu kama alivyojidhihirisha kwa Musa, Eliya na Mitume walipokuwa na Yesu.

SALA: Bwana Yesu tunaomba ndimi zetu zitumike kukusifu.