Februari 17, 2022; Alhamisi: Juma La 6 La Mwaka

Wat. Waanzilishi Saba wa Shirika la Watumishi wa Bikira Maria
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Yak. 2: 1-9
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, “Keti wewe hapa mahali pazuri”; na kumwambia yule maskini, “Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,” Je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 34: 1-6

 1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
  Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
  Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
  Wanyenyekevu wasikie wakafurahi
  K: Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
 2. Mtukuzeni Bwana pamoja name,
  Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
  Nalimtafuta Bwana akanijibu,
  Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
 3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
  Wala nyuso zao hazitaona haya.
  Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
  Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
  INJILI: Mk. 8:27-33
  Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria–Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, “Watu huninena mimi kuwa ni nani?” Wakamjibu, “Yohane Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii.” Naye akawauliza, “Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?” Petro akamjibu, akamwambia, “Wewe ndiwe Kristo.” Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, “Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

TAFAKARI
HESHIMA KWA WAKUBWA HULETA UELEWANO: Yesu aliwauliza wanafunzi wake katika ujumla wake, “Watu huninena mimi kuwa ni nani?” Bila shaka wengi hapa walijibu kwa haraka kile walichofikiria mara moja bila kujua kama wako sahihi au la! Yesu hakuwaambia kama wamepata au wamekosa. Anaporudi kwao kutaka kujua wana mtizamo gani juu yake, tunaona kazi hiyo ya kujibu wanamwachia Petro Mkuu wao ajibu. Petro anajibu kwa usahihi na Yesu anaonesha kuwa amepata “Akawaonya wasimwambie mtu”. Funzo kuu hapa ni hii heshima mitume waliyotoa kwa Petro wakitambua ndiye mkuu wao. Kuna baadhi yetu ikitokea ameulizwa jambo, atatoa majibu kama vile yeye ndiye msemaji mkuu, huku ni kuingilia majukumu ya wengine. Tuelewe kila mtu anayo heshima na majukumu fulani. Shida ni kuwa kuna wanaojipendekeza ili waonekane wao ndio zaidi au wajuaji na hivi wanaharibu mpango mzima, wanatoa majibu ambayo siyo.

SALA: Baba Mwema, tunaomba utusaidie tuweze kuwaheshimu wenye mamlaka.