Februari 16,2022 Jumatano: Juma La 6 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Yak.1: 19-27
Ndugu zangu wapenzi, mnajua kwamba kila mtu na awe mwepesi kwa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu. Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 15: 1-5

 1. Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako?
  Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, na kutenda haki,
  Asemaye kweli kwa moyo wake,
  Asiyesingizia kwa ulimi wake.
  K: Ni nani atakayefanya maskani yake
  katika kilima chako kitakatifu, Ee Bwana?
 2. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya,
  Wala hakumsengenya jirani yake.
  Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
  Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
 3. Hakutoa fedha yake apate kula riba,
  Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
  Mtu ambaye atendaye mambo hayo hataondoshwa milele. (K)

INJILI: Mk. 8: 22-26
Wakati ule, Yesu na wanafunzi wake walifika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, “Waona kitu?” Akatazama juu, akasema, “Naona watu kama miti, inakwenda.” Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. Akampeleka nyumbani kwake, akisema, “Hata kijijini usiingie.”

TAFAKARI
HATUJAUMBWA ILI TUTESEKE: Katika ulimwengu huu tunashuhudia watu wakiwa katika mateso kama magonjwa, shida na taabu mbalimbali. Mungu kwa mpango wake humpa mwanadamu karama mbalimbali za kupambana na yanayomtesa. Tunao madaktari wa kurekebisha afya zetu zinapopatwa na dhoruba ya magonjwa. Daktari anao uwezo wa kujua kuwa mtu akiugua ugonjwa fulani basi dawa yake ni hii au ile. Yesu leo anaonyesha wazi kuwa kujitibu kwa kutumia dawa halali na kwa uwazi bila kificho ni halali, sio madawa ya waganga wa kienyeji. Yesu alivyomtemea mate ili kumponya yule kipofu ni ishara tosha kuwa anao uwezo wa kuponya, angeweza kufanya vinginevyo na alifanya hivyo mara mbili kwa uwazi kungali na mwanga. Kuna wakati sisi tunaingia katika imani za kishirikina na kufanya mambo kwa kujificha tena wakati mwingine katika giza tungali uchi. Kristo leo anatuambia si vyema. Tuelewe kuwa uponyaji wa Mungu hauhiaji haraka.

SALA: Yesu mwalimu wa madaktari, tunaomba uwalinde madaktari wote.