Februari 15, 2022; Jumanne: Juma La 6 La Mwaka

Kijani
SOMO 1: Yak. 1: 12-18
Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. Mtu ajaribiwapo, asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu”; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 94: 12-15,18-19

  1. Ee Bwana, heri mtu Yule amwadibuye na kumfundisha,
    kwa sheria yako;
    Upata kumstarehesha siku ya mabaya.
    K: Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha.
  2. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake,
    Wala hutauacha urithi wake,
    Maana hukumu itarejea haki,
    Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)
  3. Niliposema, mguu wangu unateleza;
    Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
    Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu,
    Faraja zako zaifurahisha roho yangu. (K)

INJILI: Mk. 8: 14-21
Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, “Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, “Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande?” Wakamwambia, “Kumi na viwili.” “Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande?” Wakamwambia, “Saba.” Akawaambia, “Hamjafahamu bado?”

UOVU AU WEMA HUKOMAA HATUA KWA HATUA: Kuna usemi usemao “mazoea hujenga kilema”. Ukiona mtu ana tabia fulani ujue hakuzaliwa nayo, aidha alifundishwa, au alijifunza toka kwa wengine au alijizoeza kidogo kidogo. Mtu hawezi kujitetea kuwa eti nimejikuta tu nina tabia ya wizi, na hata wengine wanagiriki kusema eti amezaliwa nayo. Sio kweli, ukichunguza vizuri utakuta tangu akiwa mdogo alikuwa na tabia ya kudokoa dokoa vitu vidogo vidogo na hivyo ikawa ni mazoea yake. Waswahili husema, “Mlamba asali mwisho huchonga mzinga”. Yakobo amelielezea vizuri hili jambo kwa kusema, “Tamaa ikikua vyema huchukua mimba, nayo mimba huzaa dhambi ambayo mwisho wake ni mauti”. Tabia mbaya isipokemewa mwisho wake ni mauti.

SALA: Ee Baba utuepushe na tamaa ya dhambi.