Februari 14, 2022 Jumatatu: Juma La 6 La Mwaka

Wat. Sirili, Mtawa, na Metodi, Askofu
Kumbukumbu
Nyeupe
SOMO 1: Yak.1: 1-11
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika; salamu. Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno. Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima na aombe dua kwa mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote. Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa; bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka. Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:67, 68, 71, 72, 75, 76

 1. Kabla sijateswa mimi nalipotea,
  Lakini sasa nimelitii neno lako.
  Wewe U mwema na mtenda mema,
  Unifundishe amri zako.
  K: Rehema zako, Ee Bwana,
  zinijie nipate kuishi.
 2. Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
  Nipate kujifunza amri zako.
  Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
  Kuliko maelfu ya dhabihu na fedha. (K)
 3. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
  Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
  Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
  Sawa sawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. (K)
  INJILI: Mk. 8: 11-13
  Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, “Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki.” Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.
  UBISHI HAUNA MAANA: Kuna watu katika jamii ambao hubishana kila wakati. Kwa yote hayaendi sawa nyakati zote, hata pale ambapo wengine wanauona uwazi. Yesu katika Injili anakumbana na kundi hili la Mafarisayo. Ukweli walishaupata ila wanabishana, hawakubali, na ndipo, wanapanga kumjaribu Yesu “kutaka ishara”. Wako ambao wamekuwa wabishi hadi kifo kikawakuta katika ubishi. Mtu kwa mfano anaishi maisha bila ndoa na mwenzake, kila akishauriwa jibu lake ni kuwa anajipanga, atafunga ndoa mwakani, kila mwaka jibu lake ni mwakani, mwakani na wengine wameishia hata kifo bila kujitakasa. Hata wengine ambao nao hawana ndoa, hata wakiona mwenzao kaishia hivyo, bado hawakubali kubadilika, wanaendelea kung’ang’ania misimamo yao kuwa wanajipanga. Tutakubali lini kubadilika?

SALA: Yesu mwema tupe moyo wa kukubali kuongozwa nawe.