Februari 13,2022; Jumapili: Jumapili Ya 6 Ya Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Yer 17: 5-8
Bwana asema hivi, “Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema; bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 1: 1- 4, 6

 1. Heri mtu yule asiyekwenda
  Katika shauri la wasio haki;
  Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
  Wala hakuketi barazani pa wenye mizaa.
  Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
  Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
  (K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake,
  Wala hakuwaelekea wenye kiburi
 2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
  Kandokando ya vijito vya maji,
  Uzaao matunda yake kwa majira yake,
  Wala jani lake halinyauki;
  Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
 3. Sivyo walivyo wasio haki;
  Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
  Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
  Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 15: 12. 16-20
Wandugu wapendwa, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema ya kwamba hakuna kiyama ya wafu? Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

SHANGILIO Efe. 1:17-18
Aleluya, aleluya,
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ayatie nuru macho ya mioyo yetu,
ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.

INJILI: Lk 6: 17. 20-26
Siku ile, Yesu alisimama sehemu tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, “Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiweni siku ile na kurukaruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni; maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.”

TAFAKARI
TUMAINI LETU TUWEKE KWA BWANA KWA MAANA ANA UPENDO WA MILELE: Kutumainia wanadamu na vitu vya ulimwengu ni kama mtu anayezama majini huku amelishika ua la yungiyungi akidhani litamwokoa. Katika Injili ya Mathayo, Yesu anatangaza sera ya Ukristo katika heri nane; Injili ya Luka inatuletea heri nne na ole nne. Idadi ya heri na mpangilio si shauri la ajabu. Vyovyote iwavyo, heri zote sawa na ole zake zinatutaka tumtumainie Bwana ambaye hatatuangusha katika matumaini yetu. Kumtumaini Mungu ni kuvaa koti zuri la usalama badala ya kutegemea ua la yungiyungi.
Tukiwa tunalialia kwa magumu mbalimbali huku tukimtumainia Mungu, Mungu atatuzawadia kicheko makaoni mwake. Hata watu wakituchukia na kututenga na kutushutumu, na kuyatupa nje majina yetu kama maneno maovu, kwa sababu ya Mwana wa Adamu, tuanze kufurahi na kurukaruka, kwa kuwa thawabu yetu itakuwa kubwa mwishoni. Ndivyo walivyotendewa manabii wao wakaondokea kupata uzima wa milele na waliowadhulumu kujitia katika mtego wa kuangamia.
Injili inatuambia kuwahusu walioshikilia mali za kidunia badala ya mutegemea Mungu. Ndio wanaofurahia kushiba sasa. Mambo yatakuwa mabaya si kwa hao tu bali hata kwa wanaojitengenezea kicheko sasa pasipo kumtegemea Mungu maishani mwao. Hatimaye, wote wanaoishi wakitafuta sifa duniani, kama walivyofanya manabii wa uongo watapata kusifiwa na watu lakini mwisho wao utakuwa mbaya.
Kumtegemea Mungu ndilo jambo la maana zaidi. Watu na vitu si vya kutegemewa. Ndipo somo la kwanza likatwambia kuwa amtegemeaye mwanadamu , amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake akiwa amemwacha Bwana, ana shida. Mtu huyo atakuwa kama fukara nyikani wala hataona yatakapotokea mema. Mtu huyo atalingana na mtu anayekaa jangwani penye ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Lakini kinyume na mtu huyo ni anayemtegemea Mungu maana atabarikiwa na Bwana mwenyewe.
Somo la pili linatangaza shina la matumaini makuu ya Kikristo ndiko kufufuka kwa Yesu Kristo. Kifo kinashindwa kutokana na mshikamano na Yesu Mfufuka. Yesu asingalifufuka, matumaini ya Kikristo yasingalikuwako na Wakristo, wafuasi wa Kristo wangaliingia hasara isiyosemeka. Lakini kwa uhakika wa kuwapo kwa maisha baada ya maisha haya ndiyo maana wakimtegemea Mungu, umaskini, njaa, machozi, shutumu na vilio haviwezi kumtatiza na kumzuia Mkristo asipate uzima wa milele. Ni kwa matumaini makuu ndipo tunatawala na Kristo duniani na hatimaye mbinguni. Hili linatiwa muhuri tukiweka tumaini letu kwa Bwana. Tuchumie juani lakini mwishoni sote tulie kivulini.

SALA: Ee Mungu mwema, kusiwepo na mwingine wala kingine cha kutumaini isipokuwa wewe peke yako. Amina.