Februari 12,2022 Jumamosi: Juma La 5 La Mwaka

SOMO 1: 1Fal. 12: 26-32; 13: 33-34
Yeroboamu alisema moyoni mwake: “Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi. Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia Bwana wao, yaani, Rehoboamu mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda.”
Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng’ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, “Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri.” Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani. Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani. Tena akafanya nyumba za mahali pa juu akafanya na watu wo wote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani. Yeroboamu akaamuru kushika sikukuu katika mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi, mfano wa sikukuu iliyokuwa katika Yuda, akapanda juu ili kuiendea madhabahu. Akafanya vivyo katika Betheli akiwatolea dhabihu wale ng’ombe aliowafanya; akawaweka katika Betheli wale makuhani wa mahali pa juu alipokuwa amepafanya. Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wo wote. Kila aliyetaka akamfanya wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.

Wimbo Wa Katikati: Zab.106: 6-7, 19-22

  1. Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu,
    Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.
    Baba zetu katika Misri
    Hawakufikiri matendo yako ya ajabu.
    K: Ee Bwana, unikumbuke mimi,
    kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
  2. Walifanya ndama huko Horebu,
    Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
    Wakaubadili utukufu wao
    Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)
  3. Wakamsahau Mungu mwokozi wao,
    Aliyetenda makuu katika Misri:
    Matendo makuu katika nchi ya Hamu,
    Mambo ya kutisha kutisha penye bahari ya Shamu. (K)

INJILI: Mk. 8: 1-10
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akawaambia, “Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamjibu, “Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?” Akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakasema, “Saba.” Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie, wakawaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawaandikie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.

UKARIMU UNA FAIDA KUBWA: Mungu, baada ya kumuumba mwanadamu anamwita hapa duniani amtumikie katika maisha ya wito fulani. Kila wito una maandalizi yake, na mhusika asipokuwa na maandalizi mazuri, mbeleni kutakuwa na shida. Yeroboamu anakiuka utaratibu huu kwa kuwateua wasiotakiwa kuwa makuhani na hili linakuwa chukizo kwa Bwana. Tunaona jinsi watu wanavyoingia kwenye maisha ya ndoa bila maandalizi na hivyo ndoa hizo hazidumu. Katika injili Yesu anatuonyesha uzuri wa kuwa mkarimu. Kuna watu ambao katika maisha yao, kumpa mtu kitu au kutoa msaada ni vigumu zaidi. Ukweli ni kuwa, hakuna aliyetoa kwa ukarimu akatindikiwa na kuwa masikini. Daima kuna baraka ambazo Mungu anagawa kwa mwenye ukarimu. Kinachomsumbua mwanadamu ni ile kufikiri kuwa akitoa vinaisha, kumbe kutoa kwa moyo ni kuwekeza.

SALA: Ee Yesu utujalie moyo wa ukarimu.