Februari 11, 2022; Ijumaa: Juma La 5 La Mwaka

Bikira Maria wa Lurdi
Kijani
SOMO 1: 1 Fal. 11: 29-32; 12: 19
Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, “Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, ‘Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi; lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu, mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli.’” Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 81:9-14

 1. Usiwe na Mungu mgeni ndani yako
  Wala usimsujudie mungu mwingine.
  Mimi ndimi Bwana Mungu wako
  Niliyekupandisha toka nchi ya Misri.
  K “Mimi ndimi Bwana Mungu wako:
  isikieni sauti yangu.”
 2. Watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
  Wala Israeli hawakunitaka.
  Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,
  Waenende katika mashauri yao. (K)
 3. Laiti watu wangu wangenisikiliza,
  Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
  Ningewadhili adui zao wa upesi,
  Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu. (K)

INJILI Mk 7: 31-37
Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, “Efatha”, maana yake, “Funguka.” Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, “Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.”

TAFAKARI
KAMWE KAZI YA MUNGU HAIZUILIKI: Mungu katika mipangilio yake, akipanga jambo, lazima atalitekeleza. Ndiye mweza wa yote na mipango yote imo mikononi mwake. Alitakalo laweza kuchukua muda tofauti na yalivyo mawazo ya wanadamu. Ila tufahamu kuwa kwake Mungu hakuna lichelewalo wala lijapo kabla ya wakati wake. Alishaahidi kwa makabila kumi na mawili ya Waisraeli kuwa atakuwa nao hadi mwisho. Hata pale mfalme Sulemani anapokosa kuandamana na mpango wa Mungu, Mungu anamwinua mwingine aendeleze kazi hiyo. Licha ya kuwa Mungu hututumia sisi ili kuaiendeleza kazi zake, kamwe kazi zake hazitakwazishwa na matendo yetu. Letu ni kuwa tayari kumtumikia Mungu jinsi alivyo Yeroboamu. Tujue ya kuwa kukubali kwetu kutumiwa na Mungu ni baraka. Kukataa kutumiwa na Mungu ni kujitakia na kujiletea laana. Hivyo, tunaalikwa kuukubali ushirikiano na Mungu kama wa hawa wahusika wa injili ya leo; walimpeleka huyu kiziwi kwa Yesu ili aponywe. Tukumbuke vyema kuwa kukataa kwetu hakuzuii mpango wa Mungu, atamwinua mwingine kwa kazi hiyo.

SALA: Mungu Mwenyezi, tujalie tuwe tayari kwa kazi ya utume wako.