Februari 7, 2022; Jumatatu: Juma La 5 La Mwaka

Kijani
SOMO 1: 1 Fal. 8: 1-7, 9-13
Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la Bwana, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli walikutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng’ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la agano la Bwana hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana. Ndipo Sulemani akanena, “Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 132: 6-10

  1. Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata,
    katika konde Yearimu tuliiona.
    Na tuingie katika maskani yake,
    tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake
    K: Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako.
  2. Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako,
    Wewe na sanduku la nguvu zako.
    Makuhani wako na wavikwe haki,
    watauwa wako na washangilie.
    Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
    usiurudishe nyuma uso wa masihi wako. (K)

INJILI: Mk. 6: 53-56
Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genezareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

TAFAKARI
MSAADA KWA WENGINE NI SADAKA SAFI: Hatuwezi kukwepa kusaidiana, mwanadamu hawezi kuishi kama kisiwa, kuna mahali itafika lazima mtu atahitaji msaada wa mwingine, kamwe hakuna anayejitosheleza, tunahitajiana, mimi nitahitaji hiki nawe utahitaji kile. Katika injili tumeambiwa kuwa watu walikuwa wanawachukua wagonjwa na kuwapeleka mahali ambapo waliweza kufikiwa na Yesu. Hili ni tendo la kujisadaka na lina neema zake. Kuna watu wao kujitolea ni shida, wanasahu kuwa ipo siku nao watahitaji. Kusaidiana kunajenga jamii, kunaongeza undugu na urafiki. Kuna mwanasaikolojia alisema ‘hesabu umri wako na marafiki unaojiongezea na sio idadi ya miaka inayoongezeka’

SALA: Bikira Maria Afya ya wagonjwa, uwaombee wagonjwa wetu uponyaji-Amina.