Februari 6, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 5 Ya Mwaka

SOMO 1: Isa. 6: 1-2a, 3-8
Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita. Wakaitana kila mmoja na mwenzake, wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.” Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.” Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; Akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo akaniambia, “Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako, imefunikwa.” Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, “Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” Ndipo niliposema, “Mimi hapa nitume mimi.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 138:1-5, 7-8

 1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
  Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
  Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
  Nitalishukuru jina lako.
  (K) Ee Bwana, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
 2. Nitalishukuru jina lako,
  Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
  Kwa maana umeikuza ahadi yako,
  Kuliko jina lako lote.
  Siku ili niliyokuita uliniitikia
  Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
 3. Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru,
  Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
  Naam, wataziimba njia za Bwana,
  Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. (K)
 4. Utanyosha mkono wako juu ya hasira ya adui zangu,
  Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
  Bwana atanitimilizia mambo yangu;
  Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
  Usiziache kazi za mikono yako. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 15: 1-11
Ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.

SHANGILIO MT. 8:17
Aleluya, aleluya,
Aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu.
Aleluya.

INJILI: Lk. 5: 1-11
Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.” Simoni akajibu akamwambia, “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.

TAFAKARI
BWANA AKITUTAKA, AMETUTAKA. TUSHIRIKIANE NAYE: Bwana akitutaka tumtumikie shambani mwake ametutaka. Ana sababu yake, ana kazi yake na ana nia yake nasi. Atatutwaa tu. Katika hali hiyo ni kupatana na Bwana tu maana likikupata patana nalo. Tukubaliane na tushirikiane naye. Injili inaonyesha na inatangaza kuwa Yesu aliwataka Simoni na nduguye sawia na watoto wa Zabedayo. Tunapotakiwa na Yesu anatukuta katika hali zetu halisi. Simoni na nduguye aliwakuta katika shughuli zao za uvuvi, tena wakiwa katika shida ya ukavu wa ziwa, yaani ugumu wa kupata samaki.
Watoto wa Zabedayo aliwakuta wakisaidiana kazi yao ya uvuvi. Yesu aliwaita walivyokuwa akawatangazia, sababu na nia yake: kuwafanya wavuvi wa watu. Wakakubali wakamfuata. Wavuvi walikuwa watu wa kipato cha kuridhisha. Hivi wavuvi na watoto wa wavuvi hawakuitikia wito wa Yesu kwa ajili ya “kuganga njaa”, isipokuwa walikuwa wanaamini watakwenda kuandaliwa kwa uzima wa milele, maana ndivyo walivyofundishwa kuwa faida ya kufunzwa torati.
Wayahudi walikuwa wapesi kumfuata mtu anayejulikana atawafundisha torati kwa sababu mtu kama huyo alihesabiwa bora kuliko baba wa kimwili. Kwa nini kwa sababu alihesabiwa kuwataandalia watu uzima wa milele, uzima ulio bora zaidi kuliko uzima huu wa kimwili. Ndiyo kisa basi watoto waliweza kuwaacha wazazi wao na hata watu waliooa waliruhusiwa kuwaacha hata wake na watoto wao hata kwa mwaka mzima pasipo kuwaaga.
Iwe vyo vyote vile, kuacha yote na kuitikia mwaliko wa Mungu ni muhimu sana kwa sababu Bwana hawezi kumwita mtu kwa kumtania. Yeye huwa na sababu na nia yake. Katika somo la kwanza tunasoma Mungu alimtaka Isaya amfanye nabii kwa Waisraeli. Mungu alimtaka. Ile hali ya dhambi Isaya aliyodhani itamtatiza, Mungu aliisafisha. Kwisha kuhakikishiwa kwamba Bwana alimfanyia hivyo kwa kumtaka Isaya alikubali. Lilikuwa limempata akapatana nalo. Vivyo hivyo katika somo la pili, Mtume Paulo anatangaza kwamba alijihisi kuwa mtu asiyestahili utume lakini kwa vile Bwana alimtaka alimtokea kama nje ya muda na kwa neema yake akamfanya mtume, tena mtume aliyepata mafanikio makubwa. Bwana alimtaka. Lilimpata akapatana nalo.
Mitume walipokeza kijiti cha utume kwa watu wa wakati wao na hao wakawapasia kijiti watu wa wakati wao na hao wakawapasia wengine hadi katika karne na mwongo huu kijiti kimefika mikononi mwetu. Tumeitwa tumtangaze Mungu na Injili yake katika Nyanja mbalimbali: familia, taasisi, vigango, parokia, jimbo na ulimwengu mzima. Tukubaliane naye. Anatutaka. Kama tuna dhambi yeye mwenyewe atatutakasa kama alivyomfanyia Isaya. Kama tunadhani hatukuwa kwenye mpango asilia si kitu vile vile kwani hata Mtume Paulo alijisikia hivyo. Lakini mwishoni ni wote kukabidhiwa kazi na Bwana na tukikubaliana naye yeye mwenyewe atatumiminia neema hata tupate mafanikio makubwa.
Bwana anatutaka. Ana sababu nasi na nia nasi. Tumpe ushirikiano mkubwa naye atutunzie thawabu yetu, ndiyo uzima wa milele pamoja naye na watakatifu wake mbinguni. Wakati wowote tunapokabiliwa na Mungu ili tuingie katika mpango wake, tusifanye mioyo yetu migumu isipokuwa tuwe kama akina Isaya, mitume Simoni na Andrea, Yakobo na Yohane na mtume Paulo. Za juu ya hao wote tuwe kama Mama Bikira Maria ambaye kwa ajili ya kushirikiana na Mungu katika mradi wake wa ukombozi alisema kwa sentensi moja tu: Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena. Hilo liwe jibu letu siku zote: Sisi ni watumishi wa Bwana tutendewe tu alivyonena Bwana.

SALA: Ee Mungu tunajua kwamba unatutaka tushirikiane nawe katika mradi mkubwa wa kuwakomboa wanadamu. Tufanye tujitambue kuwa watumishi wako nawe ututendee unavyotaka. Amina.