Februari 5, 2022; Jumamosi: Juma La 4 La Mwaka

Mt. Agata, Bikira na Shahidi
Kumbukumbu
Nyekundu
SOMO 1: 1 Fal 3: 4-13
Mfalme Sulemani alienda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, “Omba utakalo nikupe.” Sulemani akasema, “Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 119: 9-14

  1. Jinsi gani kijana aisafishe njia yake?
    Kwa kutii akilifuata neno lako.
    Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
    usiniache nipotee mbani na maagizo yako.
    K: Unifundishe amri zako, Ee Bwana.
  2. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
    nisije nikakutenda dhambi.
    Ee Bwana umehimidiwa, u
    nifundishe amri zako. (K)
  3. Kwa midomo yangu nimezisimulia
    hukumu zote za kinywa chako.
    Nimefurahi njia ya shuhuda zako
    kana kwamba ni mali mengi. (K)

INJILI: Mk. 6:30-34

Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, “Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo.” Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.

TAFAKARI
SUBIRA YAVUTA HERI: Mawasiliano ambayo Sulemani alifanya na Mungu baada ya kuambiwa aombe apendalo, Sulemani hakuwa na papara, alitulia, alikuwa na subira na hivyo akaomba vyema. Mungu kwa wema wake hufanya hata zaidi ya yale tunayomwomba, anachokitaka kwetu ni kujishusha tu na kutokupenda makuu. Hata mitume katika injili tunaona kama walitaka kujisahau na kujisifia. Ndio maana Yesu anawatenga kwa faragha, hakutaka waendelee kutoa habari zake kwa uwazi ili wasiharibu yale mema waliyokwishapata. Kila mmoja wetu ana bahati yake, wahenga wanasema, “Bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi”. Sulemani aliitumia vyema bahati yake ya kuomba apendalo. Tuko ambao tukipata bahati ya namna hii sio ajabu tukaomba vitu vya ajabu na huenda tukaomba hata mambo ya kushangaza. Usishangae mtu aombapo eti fulani afe labda kutokana na kuwa na chuki naye, au unaomba gari ili uwaringishie wengine, au unaomba fulani afukuzwe kazini. Mbona tuwe na roho za chuki?

SALA: Baba yetu wa Mbinguni, utujalie daima tuombe ipasavyo hasa ya kutufaa kwa mastahili ya neema yako.