Februari 2,2022; Jumatano: Juma La 4 La Mwaka

Kutolewa Bwana Hekaluni Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mal. 3:1-4

Bwana Mungu asema hivi: “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja,” asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 24:7-10

 1. Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
  Inukeni, enyi malango ya milele.

K: Ni nani mfalme wa utukufu?
Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari.

 1. Ni nani Mfalme wa utukufu?
  Bwana mwenye nguvu, hodari,
  Bwana hodari wa vita. (K)
 2. Inueni vichwa vyenu, enyi milango,
  Naam, viinueni, enyi malango ya milele,
  Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K)
 3. Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
  Bwana wa majeshi,
  Yeye ndiye Mfalme wa utukufu. (K)

SOMO 2: Ebr. 2:14-18
Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

INJILI: Lk. 2:22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,
Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

TAFAKARI
MWANGA USITUDHURU KAMA WAGONJWA: Ibada ya kumtakasa mama ndiyo iliyofanyika kwa sadaka ya huwa au njiwa wawili, yaani siyo ile ya kumtolea mtoto. Na sisi hatushughulikii swala hilo la kutakasana kwa sababu Yesu alishalifuta kwa kusema kinachomtia mtu unajisi siyo kimwingiacho bali kimtokacho (Mk 7:14-23). Mwanga huwadhuru wagonjwa na wazima huwatia uzima. Yesu kama mwanga aliingia ulimwenguni kwa maslahi yetu. Tumwache atuangazie atutie uhai.
Kwa namna hiyo tunachoangazia macho zaidi leo ni kumtolea mtoto hekaluni. Tunathamini tukio hilo kwa sababu ndilo linalomrasimisha Yesu kuwatumikia watu wote kwa uhuru. Alipelekwa hekaluni kufanywa mlei atakayewatumikia watu wote kwa uhuru. Tukumbuke torati ilisema watoto wote wa kiume vifungua mimba wa mama zao wafanye kazi ya utumishi kama makuhani. Hata hivyo, kama mtu hakuwa wa kabila la Lawi alipaswa kuletwa hekaluni kutangazwa huru. Jambo hili ndilo linaloitwa “kutolewa hekaluni” na lilifanyika kwa kulipa pesa shekeli tano. Hivi Yesu leo analetwa hekaluni na wazazi walilipa shekeli tano kumfanya mlei atakayekuwa huru kuwatumikia watu wote akipitia njia ya mauti ya msalaba (Mk 10:41-45, Flp 2:6-11).
Kuwatumikia watu alikofanya Yesu ni sawa na kuwa mwanga kwao, kuwaangazia walio gizani, kuwafungua macho vipofu na kuwatoa gerezani wafungwa na kadhalika. Lakini kiroja cha mwanga ni kupendwa na wema na kuchukiwa na waovu. Jambo hili ndilo linalotangazwa na mzee Simeoni. Watu wema watafurahi na kujitahidi kushikamana na mwanga wakati waovu huuchukia, kuukataa na hata kuukimbia. Mkasa huo ndio utakaomuumiza sana Bikira Maria kama upanga wenye kupenya moyo wake. Yesu atakaliwa na waovu hata kumuua na kumkabidhi Maria maiti yake. Lakini wakati huo huo watu wema watakuwa wanatumia fursa hiyo kuvuna wokovu. Hao watafurahi na kumshangilia mtoto Yesu kama nuru muhimu iliyowazukia. Katika mtazamo huu, somo la kwanza linashangaa wangapi watahimili ujio wa Yesu Kristo.
Kinyume cha watu watakaomkataa Yesu ni watu watakaompokea kwa shukrani. Hao watadumu katika imani, matumaini na mapendo. Mmoja wa watu hao ni Anna. Ujane wake wa miaka 84 haukusema chochote kwake. Hakuujali na kulialia ovyo. Kifupi, hata kabla Kristo hajaanza kuhubiri Anna alizoea mapambano ya Kikristo. Kwa hiyo, alihimili ujane kwa kusali na kufunga huku akidumu hekaluni. Watawa wangependa walingane naye, ndiyo maana leo watawa wanafanya sherehe kubwa.
Sikukuu hii ituhamasishe kuukaribisha mwanga katika maisha yetu. Tuupende, utuangaze hadi tupate uzima wa milele. Kumkaribisha Yesu kwetu ni kukubali kufunzwa matunda ya roho: upendo, amani, uvumilivu, furaha, ukarimu, wema, kiasi, uaminifu na kadhalika (Gal 5:22-23). Matendo haya ndiyo yatakayotuingiza mbinguni.
Kinyume chake tutatawaliwa na matunda ya mwili, yaani matendo yatakayotuingiza jehanamu: mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi, upumbavu wanawake kubadili matumizi yanayopatana na maumbile, wanaume kuacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke – wakawakiana tamaa wao kwa wao, watu kukataa kumtambua Mungu, dhuluma, ulafi, ujuaji, ugomvi na nia mbaya; kusengenya, kusingiziana, ufidhuli, majivuno, kutowatii wazazi, kukosa dhamiri, kutotimiza ahadi, kukosa huruma kwa wengine, kuabudu sanamu, mazingaombwe (“uchawi”), uadui, hasira, mabishano, mafarakano, husuda, ulevi na mambo mengine kama hayo” (Mk 7:19-23, Rum 1:26-32, Gal 5:19-12). Kumbe, tumkaribishe Yesu kama mwanga maishani mwetu, katika familia zetu na parokia yetu, kusudi atutie uzima, tena tuwe nao tele (Yn 10:10).

SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristo, mwanga wako utuangazie usiku na mchana kusudi tuwe watu wa mwangani tukiyatenda matendo mema. Amina.