SOMO 1: Yer. 1: 4-5, 17-19
Neno la Bwana lilinijia, kusema, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke, ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao. Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”
Wimbo Wa Katikati Zab. 71:1-2, 3-4, 5-6, 15-17
(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
- Nimekukimbilia Wewe, Bwana
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe. (K) - Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda siku zote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi. (K)
SOMO 2: 1 Kor. 12:31; 13:1-13
Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma, yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
SHANGILIO Efe. 1:17,18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye. Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo, na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo.
Aleluya.
INJILI: Lk. 4:21-30
Yesu aliwaambia, “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, “Huyu siye mwana wa Yusufu?” Akawaambia, “Hapana shaka mtaniambia mithali hii, ‘Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe.”” Akasema, “Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.” Lakini, kwa hakika nawaambia, “Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu. Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika Sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.”
TAFAKARI
TUSIFADHAIKE KWA AJILI YA WATU, MUNGU ASIJE AKATUFADHAISHA MBELE YAKE: Tumwogope Mungu; tumtumikie yeye kwa moyo wetu wote pasipo kuwaogopa watu na vituko vyao. Atakayetupa tuzo la uzima wa milele ni Mungu si watu. Mungu akishatupatia kazi ya kufanya shambani mwake, tuifanye kikamilifu na kwa kujiamini. Jambo hili linaonekana katika Injili ya leo. Alipomaliza kusoma, Yesu aliwahubiria watu wa kijijini kwake pasi kuwaogopa. Hakuonea haya jambo lolote. Aliwatangazia kwamba yeye ndiye Masiya lakini hakuna kwa ajili ya matamasha ya miujiza kama wao walivyokuwa wakingojea afanye mbwembwe za miujiza mbele yao. Alikataa kukidhi matashi yao ya ovyo kwa sababu Mungu hajatujalia karama tucheze navyo kwa sifa na utukufu wetu. Mungu anaweza miujiza kufanyika ili watu wamjue, wampende, wamtumikie na mwishoni wafike kwake. Yesu hakufadhaika mbele ya watu hata kumfanya atumie maweza yake kwa maonesho. Aidha hakufadhaishwa na yeyote kiasi cha kufanywa achakachue mafundisho yake kwa ajili ya kukithi matazamio ya watu. Yesu hakuwatazama au kuwasikiliza watu ndipo awape ujumbe wanaoutarajia, bali alifanya na kufundisha ukweli ili watu wafanye kulingana nao. Utendaji wa namna hiyo ndiyo tunaopaswa kuwa nao Wakristo binafsi na Kanisa kwa ujumla. Kama ni utendaji ni kuonesha mfano. Kama ni kufundisha sisi na hata Kanisa hatupaswi kufundisha ulimwengu na kisha sisi au Kanisa lifundishe kadiri watu wanavyotaka. Si vyema mwalimu au nabii kugeuzwa mwanafunzi wa ulimwengu. Tukifadhaika namna hiyo kwa ajili ya watu, Mungu atatufadhaisha mbele yake.
Ndivyo somo la kwanza linavyosomeka vyema katika mstari huu wa mambo. Yeremia anaonywa asifadhaike mbele ya watu asije Mungu akamfadhaisha mbele yake. Ndipo aliambiwa ajikite katika kazi yake pasipo woga naye atimize utume wake kwa uimara. Hata hivyo, somo la pili linaangalisha tunatekeleza wajibu wetu pasipo kufadhaika, tufanye kwa upendo maana ndiyo mafuta ya kulainishia kauli na matendo yetu. Tusitimize wajibu zetu kwa mbwembwe na kujitafutia utukufu binafsi. Ni Mungu siyo sisi wa kutukuzwa. Hatuwezi kuutimiza utume wetu barabara tusipokuwa na upendo maana ni upendo unaoweza kutufanya tusihusudu, tusitakabari; tusijivune; tusikose adabu; tusitafute mambo yake; tusione uchungu; tusihesabu mabaya; tusifurahie udhalimu, tufurahi pamoja na kweli; tuvumilie yote; tuamini yote; tutumaini yote; tustahimili yote wakati tunamtumika Mungu na jirani. Tukitimizia upendo katika shughuli zetu ndipo tufaulu. Hatutafadhaika mbele ya watu na hivyo Mungu hatatufadhaisha mbele yake. Shime, tujitahidi maana uungwana ni vitendo.
SALA: Ee Mungu tushujaishe katika utendaji wetu. Usituache tunafadhaishwa na watu, usije ukatufadhaisha. Amina.