Januari 27,2022; Alhamisi: Juma La 3 La Mwaka

Kijani
SOMO 1: 2 Sam. 7: 18-19. 24-29
Daudi, mfalme, aliingia, akaketi mbele za Bwana, akasema, “Mimi ni nani, Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana Mungu. Nawe ulijifanyia imara watu wako Israeli, wawe watu wako milele; nawe, Bwana, umekuwa Mungu wao.
Basi sasa, Ee Bwana Mungu, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yangu, ulifanye imara milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kusema Bwana wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumwa wako, Daudi, itakuwa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii.
Na sasa Ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema; basi, Sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu, umelinena; na kwa Baraka yako, nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 132. 1-5; 11-14
K: Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, Baba yake.

 1. Bwana, umkumbuke Daudi
  Na taabu zake zote alizotaabika.
  Ndiye aliyemwapia Bwana,
  Akaweka nadhiri kwa shujaa wa Yakobo.(K)
 2. Sitaingia hemani mwa nyumba yangu,
  Wala sitapanda matandiko ya kitanda changu;
  Sitaacha macho yangu kuwa na usingizi
  Wala kope zangu kusinzia,
  Hata nitakapompatia Bwana mahali,
  Na Shujaa wa Yakobo maskani. (K)
 3. Bwana amemwapia Daudi neno la kweli,
  Hatarudi nyuma akalihalifu,
  Baadhi ya wazao wa mwili wako
  Nitawaweka katika kiti chako cha enzi. (K)
 4. Wanao wakiyashika maagano yangu,
  Na shuhuda nitakazowafundisha,
  Watoto wao nao wataketi
  Katika kiti chako cha enzi milele. (K)
 5. Kwakuwa Bwana ameichagua Sayuni,
  Ameitamani akae ndani yake.
  Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
  Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)

INJILI: Mk. 4:21-25
Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.” Akawaambia, “Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

TAFAKARI
NI VYEMA KUOMBA BARAKA KABLA YA KUANZA KAZI: Daudi anatii agizo la Mungu na hivi anajinyenyekesha na kuomba baraka kwa kazi iliyo mbele yake ambayo anaona bila Neema za Mungu hataweza, Daudi anamuomba Mungu akisema, “Neno lake alifanye imara milele”. Kwa maneno haya ni wazi kuwa Daudi alitamani kazi ya Mungu ikianza isikwame bali ikawe taa ya kudumu. Mwinjili Marko naye anasema katika injili, taa hii ya neno la Mungu iwaangazie wote. Nasi leo tunaalikwa tuwe taa kwa wote, maisha yetu yamthihirishe Kristo na hili ndilo alilofanya Mtakatifu Angela kwa kusali kila mara hadi kuanzisha shirika la masista waitwao wa Mtakatifu Ursula ambao hadi leo hii wameendelea kudumu kuwa taa iwakayo mahala pengi duniani.

SALA: Ee Mtakatifu Angela, utombee kwa Mungu tuweze nasi kuwa taa kwa wengine.