Julai 25,2022; Jumatatu: Juma La 17 La Mwaka

MT. YAKOBO, MTUME
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: 2 Kor. 4:7-15

Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu. Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 126

  1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
    Tulikuwa kama waotao ndoto.
    Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
    Na ulimi wetu kelele za furaha.

( K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha.

  1. Ndipo waliposema katika mataifa,
    Bwna amewatendea mambo makuu.
    Bwana ametutendea mambo makuu,
    Tulikuwa tikifurahi. (K)
  2. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
    Kama vijito vya kusini.
    Wapandao kwa machozi
    Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
  3. Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
    Azichukuapo mbegu za kupanda.
    Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
    Aichukuapo miganda yake. (K)

INJILI: Mt. 20:20-28

Mama yao wana wa Zebedayo alimwendea Yesu pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, “Wataka nini?” akamwambia, “Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.” Yesu akajibu akasema, “Hamjui mnaloliomba. Je! mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakamwambia, “Twaweza. Akawaambia, “Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.” Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema “Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

TAFAKARI
TUWE TAYARI KUTESEKA NA YESU KWA AJILI YA WOKOVU WETU: Leo ni sikukuu ya Mt. Yakobo Mtume. Mtume huyu alikuwa karibu sana na Yesu kiasi kuwa mamaye aliwaza kuhusu hawa vijana wake kuwa karibu naye afikapo kwenye utukufu wake. Ujirani huu kati ya Yesu na wana wa Zabedayo, ulimfanya Mtume Yakobo kuwa tayari kwa lolote hata kuutoa uhai wake kwa ajili ya Kristo. Ndiye Mtume wa kwanza kufa kifodini kati ya Mitume wote (Mdo.12:1-2). Inaonekana kuwa ombi la mama yake, ili awe na Yesu katika ufalme wake, limetimia kwa njia ya kifodini chake. Tunajifunza mambo mawili. La kwanza ni nia njema ya mama/wazazi kwa watoto wao. Je wanawaandaa vizuri kwa hilo? Na pili ni namna gani watoto wanapokea kwa upendo nia njema ya wazazi wao? Sala na nia njema ya wazazi bila jitihada ya mtoto haiwezi kuzaa matunda. Tukikumbuka sote ni vyombo vya udongo, ili tuweze kufikia malengo mema, hatuna budi kuunganisha nguvu zetu na neema na baraka za Mungu. Tuwe tayari kupokea adha zote ili tuweze kumpata Kristo.

SALA: Ee Mungu, sisi ni viumbe dhaifu, tunakuomba utuimarishe ili tukutumikie vema, Amina.