JANUARI 25,2022; JUMANNE: JUMA LA 3 LA MWAKA

KUONGOKA KWA MT. PAULO, MTUME
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mdo. 22:3-16
Paulo aliwaambia makutano, “Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihada kwa Mungu kama nyinyi nyote mlivyo leo hivi; Nikawaudhi watu wa njia hii hata kuwauwa, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake. Kama kuhani mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?’ Nikajibu, ‘Wewe u nani, Bwana?’ Akaniambia, ‘Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.’ Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, ‘Nifanye nini, Bwana?’ Bwana akaniambia, ‘Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.’ Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski. Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na wayahudi wote waliokaa huko, akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, ‘Ndugu yangu Sauli, uone.’ Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, unakawilia nini? Simama, Ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.’”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 117:1-2
K: Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

  1. Aleluya!
    Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
    Enyi watu wote, mhimidini. (K)
  2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
    Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

INJILI: Mk. 16:15-18
Yesu alionekana na wale kumi na mmoja, akawaambia, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihuburi Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
KUBADILIKA KUNAWEZEKANA: Leo Kanisa linasherehekea sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo. Mtakatifu Paulo ndiye aliyekuwa anaitwa Sauli ambaye tunaelezwa nyakati zake kabla ya kuongoka alilitesa sana Kanisa kwa kuwa kinyume chake. Lakini Mungu kwa mpango wake alimbadili na kumfanya awe chombo chake cha kueneza habari njema. Kilichomsaidia Sauli (Paulo) ni kuwa alikubaliana na mpango wa Mungu akakubali kubadilika, nasi leo tujifunze kubadilika, tusing’ang’anie maovu yetu, vionjo vyetu hasa vile vinavyotufanya tusifiwe na kupigiwa makofi angali tunaangamiza na kuumiza wengine. Tukubali kuwa wajumbe wa Neno la Mungu kama Paulo au mitume hawa ambao Kristo anawapeleka kama Injili inavyosema.

SALA: Tunaomba Ee Yesu utuangazie ili nasi tubadilike katika maisha yetu ili tutende mema.