Mt. Fransisko wa Sale, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
SOMO I: 2 Sam. 5:1-7, 10
Kabila zote za Israeli walimwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, “Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, ‘Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli.’” Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, “Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe”; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 89:19-21, 24-25
K: Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo.
- Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi,
Ukisema:
“Nimempa aliye hodari msaada,
Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu.” (K) - Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake.
Na mkono wangu utamtia nguvu. (K) - Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo
Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.
Nitaweka mkono wake juu ya bahari,
Na mkono wake wa kuume juu ya mito. (K)
INJILI: Mk. 3:22-30
Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, “Ana Beelzebuli, na kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.” Yesu akawaita akawaambia kwa mifano, “Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele; kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.”
TAFAKARI
MUNGU HUSIMAMA NA ALIOWACHAGUA: Katika masomo ya leo tunapata nafasi ya kunukuu yaliyofanyika katika Agano la Kale na lile Jipya. Katika somo la kwanza tunamuona Daudi akiwa Hebroni. Wazee wa Israeli wanamwendea na kumkumbusha aliyosema Bwana, “Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli.” Wanamtawaza Daudi ili kutimiza maneno aliyoyasema Mungu. Katika wimbo wa katikati, Daudi anatukuzwa na Mungu kwa maneno, “Nimemwona Daudi, mtumishi wangu. Nimempaka mafuta yangu matakatifu.” Tunapoangalia injili ya leo, tunampata Yesu akiwaeleza waandishi ya kuwa nguvu zake zatoka kwa Mungu. Waandishi wanamlaumu Yesu eti anatumia nguvu za Beelzebuli. Katika kufanya hivyo wanamkashifu Mungu, kwani ndiye chanzo cha nguvu zake Yesu. Mungu anajidhihirisha kupitia kwa matendo yake Yesu aliye na imani kuu kwake Mungu baba yake. Je! Sisi tunayo imani kwake Mungu? Tunapokumbwa na changamoto, tunayo imani kamili kumtumainia Mungu tukifahamu vyema kuwa yu nasi kila wakati?
SALA: Mungu, tuwezeshe tuwe na imani kuwa u nasi kila wakati.