Januari 23,2022; Jumapili: Jumapili Ya 3 Ya Mwaka

SOMO 1: Neh. 8:2-10
Watu wote walikusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha torati ya Musa, Bwana aliyowaamuru Israeli. Naye Ezra, kuhani, akaileta torati mbele ya kusanyiko, la wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakakisikiliza kitabu cha torati. Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Mishaeli, na Milkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu.
Ezra akakifungua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, “Amina, Amina”, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi. Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa. Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, “Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie.” Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. Kisha akawaambia, “Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu, maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 19:7-9, 14
(K) Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu;
maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.

 1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
  Huiburudisha nafsi.
  Ushuhuda wa Bwana ni amini,
  Humtia mjinga hekima.(K)
 2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
  Huufurahisha moyo.
  Amri ya Bwana ni safi,
  Huyatia macho nuru. (K)
 3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
  Kinadumu milele
  Hukumu za Bwana ni kweli,
  Zina haki kabisa. (K)
 4. Maneno ya kinywa changu,
  Na mawazo ya moyo wangu,
  Yapate kibali mbele zako Ee Bwana,
  Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 12:12-30
Kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwanyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe.
Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?

SHANGILIO Lk. 4:18-19
Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma, kuwahubiri maskini habari njema,
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao,
Aleluya.

INJILI: Lk. 1: 1-4; 4: 14-21
Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu, kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu, upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.
Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akaenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya Sabato akaingia katika Sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha Nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza Mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Akakifunga Chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”

TAFAKARI
TUAMBIANE UKWELI MUNGU ATUPENDE: “Msema ukweli ni mpenzi wa Mungu”. Hivi tuambiane ukweli Mungu atupende. Jambo hili linapatikana katika Injili na linaungwa mkono na masomo mawili yanayoisindikiza. Kabla ya kusema mengi, tuanzie mbali kidogo. Tuchungulie mambo yalivyokuwa katika jamii ya Wayahudi. Wao walileana na kujilea katika kuyajua Maandiko Matakatifu (Torati). Kwa kuwa waliamini kwamba dini ni wajibu wa wanaume, kadiri walivyotafsiri Kum 6:7, waliwakamata sana watoto wa kiume. Walipoanza kusema mama na wakubwa wa familia waliwafundisha kusali, hususan sala ya Shema, papo hapo waliwapeleka chekechea walikofundishwa kuandika, kusoma na kuhesabu. Vijana hao walipofikia miaka 12 walipelekwa hekaluni kwa sherehe ya kuidhinishwa kwamba wamekuwa wakubwa kidini (bar mitsheva).
Kwa namna hii, Wayahudi wanaume wote waliweza kushiriki katika kusoma na kufafanua Maandiko katika mkutano wa sala iwe hekaluni au kwenye sinagogi. Ndiyo tunavyoona jinsi anavyoshiriki Yesu leo. Myahudi mwanaume alipofika kwenye sinagogi alikuwa tayari kusoma Maandiko akichaguliwa kusoma somo la kwanza kutoka kimojawapo ya vitabu vya Torati na alikuwa tayari kusoma na kuhubiri akichaguliwa kusoma somo la pili kutoka kitabu chochote cha manabii. Tunasikia Yesu alichaguliwa kusoma somo la pili, hivyo licha ya kusoma alihubiri. Kama nabii aliwahubiria ukweli. Hata hivyo huko inakokatikia Injili kumejificha jambo la kusikitisha kwamba wasikilizaji hawakuvumilia ukweli wa kuwachoma. Watu wa kwao wakamkataa nabii wao. Walikereka nao wakataka kumuua mhubiri jumla. Mambo yamekuwa mazuri sana katika somo la kwanza.
Baada ya kuitupa Torati na kuishi kwa muda mrefu maisha mapujufu, vitabu vya Torati vinagunduliwa na Wayahudi wanasomewa na kuhubiriwa katika hadhara. Wakaambiwa ukweli, watubu na wajirudi. Maneno yakawakolea, wakaambilika. Wakaahidi kuachana na maisha yao ya hatari. Wakaahidi kuishi maisha maadilifu mbele ya Mungu. Huko mbele walibadilikaje si shauri la kuhangaikia hapa. Lakini, kwa jinsi yoyote, tukiutazama mwanzo huo, walifanya vizuri sana na laiti na sisi tungeukubali ukweli wa kuhamasishwa na kuonywa kama wao. Ni katika wororo wa moyo wa namna hiyo tungefuzu kutumia vyema karama zetu zinatangazwa katika somo la pili kwamba kila mtu amepewa.
Roho Mtakatifu alivyo mkarimu, hakuna mwanadamu aliyenyimwa karama na kuachwa, bali kila mmoja ana karama ambayo akiivumbua au akisaidiwa kuivumbua anaweza kuwafaidia wengine na mwenyewe pia. Tusipoukubali ukweli kwamba tumepewa karama mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia, tutaangukia kwenye majivuno, ubinafsi na kiburi, vitu ambavyo vitasababisha siyo tu Mungu kuingia hasara kwa kutujalia karama ambazo haziwafaidi watu bali tutakula hasara ya sisi wenyewe kukataliwa mwishoni mwa maisha haya. Tujihadhari kabla ya ajali. Si vyema kujaliwa neno la Mungu na kulisikia halafu kuambulia patupu.

SALA: Ee Mungu tusaidie tuwe na masikio na mioyo miororo ili tuupende ukweli unaotufikia kupitia Maandiko Matakatifu kusudi tubadilike na wewe utupende. Amina.