Januari 22,2022; Jumamosi: Juma La 2 La Mwaka

Mt. Vinsenti, Shemasi na Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO I: 2 Sam. 1:1-4, 11-12, 17-19, 23-27
Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi; hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia. Daudi akamwambia, “Umetoka wapi?” Akamwambia, “Nimeokoka katika kambi ya Israeli.” Daudi akamwambia, “Yalikwendaje? Tafadhali uniambie.” Akajibu, “Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.” Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua; na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana, na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga. Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya: “Wana wa Yuda na wafundishwe haya, walio fahari yako, Ee Israeli, juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; jinsi mashujaa walivyoanguka! Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza maishani wala mautini hawakutengwa; walikuwa wepesi kuliko tai, walikuwa hodari kuliko simba. Enye binti za Israeli, mlilieni huyo Sauli, ambaye aliwavika mavazi mekundu kwa anasa, akazipamba nguo zenu dhahabu. Jinsi mashujaa walivyoanguka katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa juu ya mahali pako palipoinuka! Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, ulikuwa ukinipendeza sana; upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, kupita upendo wa wanawake. Jinsi mashujaa walivyoanguka, na silaha za vita zilivyoangamia!”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 80:1-2, 4-6
(K) Ee Mungu, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

 1. Weweuchungaye Israeli, usikie,
  Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi.
  Wewe uketiye juu ya Makerubi, utoe nuru.
  Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase,
  Uziamshe, utuokoe. (K)
 2. Ee Bwana, Mungu wa majeshi,
  Hata lini? Utayaghadhibisha maombi ya watu wako?
  Umewalisha mkate wa machozi,
  Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.
  Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu,
  Na adui zetu wanacheka wao kwa wao. (K)

INJILI: Mk. 3: 20-21
Yesu aliingia nyumbani na mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

TAFAKARI
KUNA BARAKA KATIKA KUWAOMBEA WAFU: Daudi anasikitika, anawaombolezea na kuwalilia Sauli na Yonathani waliofariki. Ni tabia yetu Wakristo kuwaombea wafu wetu hasa wale tulioishi nao kwa ukaribu kama ilivyokuwa kwa Sauli, Yonathani na Daudi. Katika kuwaombea kunatustahilisha neema kwa kifo chetu. Hata Yesu alimlilia rafiki yake Lazaro baada ya kusikia amefariki. Daudi anakumbuka upendo aliotendewa na Yonathani wakati wa uhai wake. Hapa tunapata fundisho la kuenzi yale mema tunayotendewa na wenzetu baada ya kufariki kwao. Tuko ambao mwenzetu akishafariki tunayokumbuka ni yale mabaya tu na hivyo hata kupelekea kufurahia kufa kwao.

SALA: Ee Yesu utujalie kuenzi mema yaliyotendwa na waliotutangulia.