Januari 20,2022; Alhamisi: Juma La 2 La Mwaka

Mt. Fabiano, Papa na Mt. Sebastiano, Mashahidi
Kijani
SOMO I: 1 Sam 18:6-9; 19:1-7
Walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe na vinanda.
Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, “Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu yake.” Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, “Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?” Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, “Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lolote nitakuambia.” Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye, akamwambia, “Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi; kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?” Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, “Aishivyo Bwana, yeye hatauawa.” Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 56:1-2, 8-12
K: Nimemtumaini Mungu sitaogopa.

 1. Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza
  Mchana kutwa ananionea akileta vita.
  Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa,
  Maana waletao vita yangu kwa kiburi ni wengi,
  Ee Mungu wangu. (K)
 2. Umehesabu kutangatanga kwangu,
  Uyatie machozi yangu katika chupa yako,
  Je! Hayumo katika kitabu chako?
  Ndipo adui zangu watarudi nyuma
  siku hiyo niitapo. (K)
 3. Neno hili najua kuwa Mungu yu upande wangu.
  Kwa msaada wa Mungu nitalisifu neno lake,
  Kwa msaada a Bwana nitalisifu neno lake. (K)
 4. Nimemtumaini Mungu,
  Sitaogopa mwanadamu atanitenda nini?
  Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu,
  Nitakutolea dhabihu za kushukuru. (K)

INJILI: Mk. 3: 7-12
Yesu alijitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.

TAFAKARI
WIVU HAUJENGI: Kwa jinsi Mungu alivyoumba, kila mmoja analo la kutimiza hapa duniani. Wakati mwingine tunaharibu baraka zinazotokana na lile tulilofanya kutokana na kujilinganisha na wengine. Hata twajua sadaka ya Kaini haikupata kibali kama ya Abeli kwa sababu aliona wivu hadi kukasirika. Hali kama hii inaharibu sana utume, kazi, na hata mwelekeo wa familia. Wapo wanaoshindwa kufanya utume wao kutokana na kukodolea macho utume wa mwenzake, familia haiendelei kutokana na kujilinganisha na familia ya pembeni. Kuna padre mmoja alimfitini padre mwenzake kwa viongozi wa juu ili ahamishwe kutokana na yeye kuwa na mvuto na watoto wa parokia ile waliyokuwa wanafanya utume pamoja. Hali kama hii inaondoa upendo wa kindugu. Hali hii ndiyo iliyomkuta Sauli, anashindwa kuelewana na Daudi baada ya utume wa Daudi kuwa na mwelekeo tofauti na wa kwake, hadi anapanga kumdhuru. Hili linachochewa na kuwa na wivu.

SALA: Mungu Mwenyezi tujalie turidhike na utume wetu na utuepushe na wivu.