Juni 30,2022; Alhamisi: Juma La 13 La Mwaka

Wat. Mashahidi wa Kwanza wa Kanisa la Roma
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Amo. 7: 10-17

Amazia kuhani wa Betheli, alipeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, “Amosi amefanya fitina juu yako kati ya yumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote.” Kwa maana Amosi asema hivi, “Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake.” Tena Amazia akamwambia Amosi, “Ewe mwana, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme.” Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, “Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi”; Bwana akaniambia, “Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.” Basi, sasa lisikie neno la Bwana; Wewe unasema, “Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka; kwa hiyo,” Bwana asema hivi, “Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe nwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 19:7-10

 1. Ushuhuda wa Bwana ni amini,
  Humtia mjinga hekima.
  Maagizo ya Bwana ni adili,
  Huufurahisha moyo.

K: Hukumu za Bwana ni kweli, na ni za haki kabisa.

 1. Amri ya Bwana ni safi,
  Huyatia macho nuru.
  Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
  Kinadumu milele. (K)
 2. Hukumu za Bwana nu kweli,
  Zinz haki kabisa. (K)
 3. Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
  Kuliko wingi wa dhahabu safi.
  Nazo ni tamu kuliko asali,
  Kuliko sega la asali. (K)

INJILI: Mt. 9:1-8

Yesu alipanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, “Jipe moyo mkuu, mwanangu; umesamehewa dhambi zako.” Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, “Huyu anakufuru.” Naye Yesu hali akijua mawazo yao, akasema, “Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende?’ Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako.” Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.

TAFAKARI
UTAKUWA NABII KWA WATU WANGU: Amazia anamlaumu Amosi kuwa nabii wa uwongo anayetafuta maslahi yake na anachochea Amosi afukuzwe. Amosi anasimama kidete na kujitetea kwamba ameitwa na Mungu kwa ajili ya Israeli. Aliendelea bila woga kutoa unabii. Aliendelea kuhubiri toba kwa kufuata maagizo ya Bwana na kuwafumbua waisraeli macho, ili kuwaepusha na hukumu za Bwana. Kristo anamsamehe na kumponya aliyepooza, na kujidhihirisha kama nabii anayewaletea maskini habari njema; ‘nimekuja ili wawe na uzima,’ alisema. Nabii Amosi ni sauti ya Mungu kwa taifa la Mungu. Kristo ni Neno wa Mungu kwa Mataifa. Wanakabiliana na upinzani, hawasiti kuwahubiria watu uzima na Toba.
Waumini wanahimizwa kusikiliza sauti ya Mungu kupitia kwa mitume wake. Watumishi wa Mungu nao wawe na ujasiri na watangaze ukweli na toba, hata kama wanakumbana na changamoto, sio kwa masilahi yao wenyewe, bali kwa ajili ya kulikomboa Kanisa la Mungu.