Januari 17,2022; Jumatatu: Juma La 2 La Mwaka

Mt. Antoni, Abati
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO I: 1 Sam. 15:16-23
Samweli alimwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia. Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana. Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali. Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kuitii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 50:8-9, 16-17, 21, 23
K: Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

 1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
  Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
  Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
  Wala beberu katika mazizi yako. (K)
 2. Una nini wewe kuitangaza sharia ya yangu,
  Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
  Maana wewe umechukia maonyo,
  Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
 3. Ndivyo ulivyofanya, name nitanyamaza;
  Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
  Atoaye dhabihu za kushukuru,
  Naye autengenezaye mwenendo wake,
  Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)

INJILI: Mk. 2:18-22
Siku moja wanafunzi wake Yohane na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, “Kwani wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.”

TAFAKARI
UTII NI MWANZO WA KUPATA BARAKA: Katika somo la kwanza, Samweli anajaribu kumfafanulia Sauli jinsi alivyo. Kukiuka utaratibu aliopewa na Mungu na hivyo mpango mzima wa Mungu kwa Wana wa Israeli unavurugika. Hata nasi katika misha yetu kuna nyakati tunakaidi na hivyo kukosa mengi. Kukosa utii kunaziba masikio ya usikivu, kunaleta kiburi, kujiona, kudharau, kuwa na ukatili na kutojali. Hata wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Eva) walikosa utii na hivyo wakaanguka katika dhambi ya Asili. Mtu kukosa utii kunapelekea hata kutotimiza wajibu. Kuna usemi usemao, “utii ni bora kuliko sadaka”. Kwa kifupi twaweza kusema, utii ni ukamilifu wa mengi na ni chanzo cha maelewano hasa kwa maisha ya jumuiya.

SALA: Ee Baba tuwezeshe kutii bila shuruti.