Januari 16,2022;Jumapili: Jumapili Ya 2 Ya Mwaka

SOMO 1; Isa. 62:1-5
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa. Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.

Wimbo Wa Katikati Zab. 96:1-3, 7-10
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Mwimbieni Bwana nchi yote.
  Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. (K)
 2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku,
  Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
  Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
 3. Mpeni Bwana enyi jamaa za watu,
  Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
  Mpeni Bwana utukufu wa jina lake. (K)
 4. Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu,
  Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
  Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
  Atawahukumu watu kwa adili. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 12: 4-11
Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.

SHANGILIO Yn. 8:12
Aleluya, aleluya,
Yesu aliwaambia akasema: “mimi ndimi nuru ya ulimwengu, Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
Aleluya.

INJILI: Yn. 2: 1-12
Wakati ule, palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, “Mama tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.” Mamaye akawaambia watumishi, “Lo lote atakalowaambia, fanyeni.” Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa Desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, “Jalizeni mabalasi maji.” Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, “Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza.” Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, “Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.” Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. Baada ya hayo akashuka mpaka Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake; wakakaa huko siku si nyingi.

TAFAKARI
UUNGWANA NI KUFANYA LOLOTE TUNALOAMBIWA NA YESU: Tukio la harusi ya Kana ni tukio la tatu la Epifania. Yesu anafanya muujiza wake wa kwanza kwa ajili ya kujidhihirisha na ndiyo maana mioyo ya wanafunzi ilifunguliwa wakamwamini. Huko nyuma ameshaonekana kwa wachungaji, mamajusi, na watu waliokuwa wakibatizwa kwa Yohane Mbatizaji. Katika Epifania hii anaonekana kwa watumishi wa harusini Kana na wanafunzi. Na bila shaka baaada ya kuufanya muujiza wake hata wale waliokunywa divai yake nzuri pasipo kumtambua yeye na Bikira Maria, waliweza kumtambua. Hii ina maana kuwa kujitambulisha kwa Yesu Kristo kumeshapindukia mipaka ya watu wa kada zote au wa shughuli zote. Alishatambulishwa kwa wanyonge (wachungaji), wataalamu (mamajusi), watu wa dini (makuhani na wakubwa wao), wenye dhambi (watu waliokuwa wanabatizwa na Yohane Mbatizaji). wafanyakazi (watumishi wa harusini), wanandoa na wanafamilia (walioona Kana), wenye furaha (waliohudhuria harusi) na wanafunzi wa Yesu. Ndipo somo la kwanza linasema kwa haki, katika Israeli kumefika nuru ya kuangazia watu. Watu hao wamefikishwa kwenye hadhara ya wokovu. Yeyote atakayepotea atapaswa kujilaumu mwenyewe kwa kutowajibika kwa nuru hiyo.
Kujidhihirisha kwa Yesu kwa kada mbalimbali za watu kunakwenda sawa na nia ya Roho Mtakatifu kuwagawia watu karama mbalimbali kusudi watumikiane kama viungo vya mwili vinavyotumikiana, na mwishoni mwa kutumikiana huko kila mmoja awe na uwezekano wa kupata uzima wa milele. Wanadamu hawapewi karama kwa ajili ya kudharauliana, kuumizana na hata kuangamizana. Karama ni kwa ajili ya kuhudumiana, kupendana na kupelekana kwenye uzima wa milele.
Haijalishi kuwa hatukuwa kule Bethlehemu alikolala horini, mtoni Yordani alikokuwa akibatizwa na hata harusini Kana, kushiriki kwetu kwenye masomo leo, tukiwa watu wenye imani, basi timeshiriki uonyesho wa Yesu. Tusipomtambua, kumsikiliza na kufanya anavyotuagiza, hasara ya roho tutakayopata itakuwa shauri letu wenyewe.

SALA: Ee Mungu mwema, tusaidie tumtambue Yesu Kristo mwanao, katika nafasi ya jamii yoyote tuliyomo na katika hali yoyote tuliyomo, mamoja iwe ya dhiki au furaha. Amina.