Januari 12,2022; Jumatano: Juma La 1 La Mwaka

SOMO I: 1 Sam. 3:1-10, 19-20
Mtoto Samweli alimtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, “Mimi hapa.” Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, “Mimi hapa; kwa maana uliniita.” Akasema, “Sikukuita; kalale tena.” Naye akaenda, akalala tena. Bwana akaita mara ya pili, “Samweli! Samweli!” Akaondoka akamwendea Eli, akasema, “Mimi hapa; kwa maana uliniita.” Akajibu, “Sikukuita, mwanangu; kalale tena.”
Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, “Mimi hapa; kwa maana uliniita.” Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli, “Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, ‘Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.’” Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, “Samweli! Samweli!” Ndipo Samweli akasema “Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.” Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini. Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 40:1, 4, 6-9
K: Tazama nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Bwana.

  1. Nalimngoja Bwana kwa Saburi,
    akaniinamia akakisikia kilio changu.
    Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake,
    wala hakuwaelekea wenye kiburi
    wala hao wanaogeukia uongo.(K)
  2. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
    Masikio yangu umeyazibua,
    Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
    Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
  3. Katika gombo la chuo imeandikwa,
    kuyafanya mapenzi yako,
    Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu,
    Naam, sharia yako imo moyoni mwangu. (K)
  4. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
    Sikuizuia midomo yangu, Ee Bwana, unajua. (K)

INJILI: Mk. 1: 29-39
Siku ile, Yesu alipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohane. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, “Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea.” Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.

TAFAKARI
MALEZI NI KAZI ENDELEVU: Sehemu nyingi watu wanalalamika kuwa vijana wamepotoka, mmomonyoko wa maadili. Kijana Samweli tunaona hachoki kuamka na kwenda kwa Eli kuuliza kama amemwita. Hii ni dalili wazi ya kukubali kulelewa. Kuna vijana wengine leo hii hata ukiwaita hawaitikii na si ajabu wakakurudishia tusi, ‘we mzee umepitwa na wakati, chukua zako time’. Eli naye kwa upande wake pamoja na uchovu wote wa usiku, hakuona kuwa Samweli anamsumbua. Hapa wazazi na walezi tujifunze kutochoka kulea, kazi ya kulea ni endelevu. Jumuiya ya wazazi Tanzania imetoa kitabu chenye kichwa cha habari “kuporomoko kwa maadili Tanzania” katika kitabu hiki sura ya pili wamesema hivi “wazazi hufundisha watoto wao mambo mengi, jinsi ya kula, kusalimiana, kufanya kazi…”rejea ukurasa wa 24. Hili alilifanya Eli kwa Samweli na hivi akamsaidia kuitikia sauti ya Mungu.

SALA: Baba wa Mbinguni, tunaomba uwajalie vijana wetu Neema ya kukubali malezi.