Januari 10,2022; Jumatatu: Juma La 1 La Mwaka

SOMO I: 1 Sam. 1:1-8
Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, Mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu; naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja aliitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi Dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, humpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi kwa hivyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, “unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 116:12-14, 17-19
K: Nitakutolea dhabihu ya kushukuru.

 1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie
  Visiwa vingi na vifurahi.
  Haki na hukumu ndiyo msingi wa kiti chake. (K)
 2. Mbingu zimetangaza haki yake,
  Na watu wote wameuona utukufu wake.
  Enyi miungu yote, msujuduni Yeye. (K)
 3. Maana Wewe, Bwana, ndiwe uliye juu,
  Juu sana kuliko nchi yote;
  Umetukuka sana juu ya miungu yote. (K)

INJILI: Mk 1:14-20
Baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu alienda Galilaya, akiihubiri Habari njema ya Mungu, akisema, wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, “Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.

TAFAKARI
MAISHA YA NDOA YANAHITAJI UVUMILIVU NA KUJISADAKA: Somo la kwanza leo limebeba ujumbe mzito sana hasa kwa wanandoa, wapo wanaodhani kuwa maisha ya ndoa ni rahisi, kila mmoja ana dhana tofauti kuhusu ndoa, wapo wanaochukulia kuwa kuoa mke ni kwa ajili ya kumpata mfanyakazi wa shughuli za ndani kama kupika, kufua, usafi nk na wengine wanachukulia ni kwa ajili ya kuzaa watoto hivyo kwamba haya anayoyafikiria ambayo kwayo ndio maana kaoa yasipotimizwa basi, ndoa inasambaratika. Elkano wa somo la kwanza leo anawaasa wanandoa kuchukulia maisha ya ndoa katika mtizamo mwingine hasa wa kuwa na utu na kumjali mwenzi wako wa ndoa, kuwa wa faraja na hasa inapotokea shida au tatizo kwa mmojawapo basi mwingine awe kitulizo “kwani huli chakula?, kwani moyo wako una huzuni?” Tunaalikwa leo tumfuate Yesu katika maisha anayotuitia kama wanandoa, tuige mfano wa hawa wafuasi wa Injili ya leo walivyoitikia mara wakamfuata Yesu na hivi wakabarikiwa.

SALA: Baba tunaomba daima uwabariki wanandoa waishi vyema viapo vyao.