Januari 9,2022; Jumapili: Ubatizo Wa Bwana

SOMO 1: Isa. 42:1-4, 6-7
Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

Wimbo Wa Katikati Zab. 29:1-4,9-10
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

 1. Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
  Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
  Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
  Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu (K)
 2. Sauti ya Bwana I juu ya maji
  Bwana yu juu ya maji mengi
  Sauti ya Bwana ina nguvu,
  Sauti ya Bwana ina adhama. (K)
 3. Sauti ya Bwana yawazalisha ayala.
  Na ndani ya hekalu lake wanasema wote, Utukufu.
  Bwana aliketi juu ya gharika;
  Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)

SOMO 2: Mdo. 10: 34-38
Siku ile: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.” Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli, akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo ( ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

SHANGILIO Mk. 9:7
Aleluya, aleluya,
Mbingu zilifunguka na sauti ya Baba ikasikika, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”
Aleluya.

INJILI: Lk. 3:15-16, 21-22
Siku ile: watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohane, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohane alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili; kama hua; sauti ikatoka mbinguni, ‘Wewe ndiwe Mwanagu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.’

TAFAKARI
MTU YEYOTE AMCHAYE MUNGU NA KUTENDA HAKI HUKUBALIWA NAYE: Ukweli na siri ya wazi ni kwamba Mungu hana upendeleo isipokuwa katika kila kabila mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa naye. Hayo ndiyo tunayotangaziwa leo na Injili inayotusimulia Epifania ya pili. Katika sherehe rasmi ya Epifania tuliona jinsi Mungu alivyojionesha kwa mataifa katika tukio na mamajusi kufika Bethlehemu na leo Yesu Kristo anaoneshwa kwa watu wengi waliokuwa kwa Yohane Mbatizaji wakibatizwa. Kwa Yohane Mbatizaji walikuwapo watu wenye njaa ya toba waliofika kutoka kona mbalimbali za nchi yao kubatizwa katika maji. Kwa ujumla wao watu hao walikuwa wadhambi.
Luka anawaorodhesha kama watoza ushuru na wadhambi wengine (Lk 3:1-22) ambao kadiri ya mafundisho ya Wayahudi walikuwa makahaba, wachungaji, askari na washona viatu. Yohane alimdokeza Yesu akiwafundisha watu kwamba mtu mkubwa kupita yeye alishafika ulimwengu awabatize watu kwa moto na roho kwa kusudi la kuwaongoza kwenye uzima wa milele. Hapo alimtangaza kwa kadamnasi ile Yesu anayekuja kuwabatiza kwa Ubatizo wa kisakramenti na hivyo kuwasafisha dhambi na maovu yao yote kwa Roho Mtakatifu na moto. Alipokwisha kubatizwa Yesu, Mungu akamfunua kikamilishwa akimtangaza kuwa mwanawe, mpendwa wake anayependezwa naye.
Jumla ya maneno ya Yohane Mbatizaji na kauli ya Mungu ni Epifania ya pili. Mungu anawataka wadhambi wote, kila mmoja kwa ubaya wake, kumtambua Yesu Kristo na hivyo kuamua kuachana na jana yake ya ubaya aingie katika leo inayoongoza kwenye uzima wa milele.
Ndiyo maana somo la kwanza linatangaza sifa za Yesu Kristo, Masiha wa Bwana, akitajwa kuwa nuru ya mataifa, anayeingia ulimwenguni ayafunue macho ya vipofu, awatoe gerezani waliofungwa na awatoe walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa. Sifa hizi zote zinaonyesha jinsi mradi wa Mungu ulivyolengwa katika kuwapata watu wa aina zote, hususan wadhambi na wenye dhiki. Hakuna mwanadamu yeyote anayeachwa nje ya mpango huo. Na ni kwa kisa hiki Mungu hajawalenga wateule fulani tu. Jambo hilo hata mtume Petro aling’amulishwa ndipo akasema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”
Wanadamu wote tuupokee mpango wa Mungu wa kutukomboa. Wanaojisikia hawana dhambi (ingawa wanajidanganya – 1Yoh 1:8-10) sawia na wanaojitambua kuwa na dhambi tuache masihara, tuukamate mwaliko wa kuanza safari na Yesu Mwokozi wetu. Mungu ametukusudia tulie kivulini, basi tusiogope hata kidogo gharama ya kuchumia kwetu juani.

SALA: Ee Bwana Mungu wetu, tujalie mioyo mikunjufu na yenye kutubu na kusikia kusudi nasi tuwepo kati ya watoto wapendwa, unaopendezwa nao. Amina.