Januari 7,2022; Ijumaa: Baada Ya Epifania

Raymundi wa Penyafort, Padre
SOMO 1: 1 Yn. 5:5-6, 8-13
Wapenzi: mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. Kwa maana wako watatu washuhudiao (mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha wako watatu washuhudiao duniani), Roho na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe. Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini jina la Mwana wa Mungu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 147:12-15, 19-20
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

 1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
  Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
  Maana ameyakaza apingo ya malango yako
  Amewabariki wanao ndani yako. (K)
 2. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
  Akushibishaye kwa unono
  wa ngano.
  Huipeleka amri yake juu ya nchi;
  Neno lake lipiga mbio sana. (K)
 3. Humhubiri Yakobo neno lake,
  Na Israeli amri zake na hukumu zake.
  Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
  Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

INJILI: Lk. 5:12-16
Ikawa Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, “Bwana ukitaka, waweza kunitakasa.” Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, “Nataka; takasika.” Na mara ukoma wake ukamwondoka. Akamkataza asimwambie mtu, ila, “Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao.” Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.

TAFAKARI
KUOMBA KWA IMANI: Mhusika tunayeelezwa katika Injili aliamini kuwa Yesu anaweza kumponya na ukoma wake. Jambo zuri tunalojifunza hapa ni kuwa mhusika hakumlazimisha Yesu amponye, alimwachia uhuru aamue mwenyewe, “Bwana ukitaka waweza kunitakasa”. Wakati mwingine sisi tumekuwa tukiomba na hatufanikiwi kwani tunalazimisha au tunaweka masharti. ‘Ee Mungu nipe 1,2,3 ili nimtambishie fulani, hatuombi kwa unyenyekevu na kujishusha au tunaomba tukiwa tushajihakikishia kuwa tutapewa na ndio maana tunakosa subiri. Mtu analeta ombi asubuhi anataka jioni apate jibu. Yesu baada ya kukubali ombi lake anamwelekeza la kufanya, ‘kutoa shukrani’. Sisi huenda hatutoi shukrani baada ya kutimiziwa. Wahenga husema “kushukuru ni kuomba tena” Kutoshukuru ni kujisahau, ni kuona kuwa tulichopata ni kwa uwezo wetu au ni haki yetu.

SALA: Bwana tujalie tuwe na moyo wa kushukuru.