Januari 6,2022; Alhamisi: Baada Ya Epifania

SOMO 1: 1Yn. 4:19-5:4
Wapenzi: Sisi twampenda Mungu kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza. Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.
Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye. Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito. Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 72:1-2, 14-15
K: Mataifa yote ya dunia watakusujudia, Ee Bwana.

 1. Ee MUngu, mpe mfalme hukumu yako,
  Na mwana wa mfalme haki yako.
  Atawaamua watu wako kwa haki,
  Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
 2. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu,
  Na damu yao ina thamani machoni pake.
  Na wambombee daima ;
  Na kumbariki mchana kutwa. (K)
 3. Jina lake na lidumu milele,
  Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
  Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
  Na kumwita heri. (K)

INJILI: Lk. 4:14-22
Siku ile, Yesu alirudi kwa nguvu za Roho, akaenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake.

TAFAKARI;
MAISHA YA UPENDO YANAHITAJI ILI KUJITOA SADAKA: Kuna mwanasaikolojia anayeitwa Johann K. Lavater aliyesema, “Yeyote anayemdanganya mwenzake kwa kujua, atamdanganya pia Mungu wake”. Nimependa kunukuu usemi wake huu nikilenga ujumbe anaotoa Yohani katika somo la kwanza, kuwa kama hatumpendi binadamu mwenzetu tunayeishi naye na kumwona hatuwezi kumpenda Mungu. Kumbe basi, Mungu huonekana katika ndugu zetu na hii inaturudisha katika uumbaji kuwa kila mtu kabeba sura na mfano wa Mungu. Na hili ndilo lililowashangaza wahusika tunaoelezwa katika Injili kuwa, “walimkazia macho”. Hii ni kutokana na ukweli kuwa Yesu aliwafanya waone ukuu wa Mungu kwa yale aliyosema. Ni kama walikuwa wamebumbazwa, aliwafumbua macho, ni kama vile walikuwa gizani. Kukaza macho ndani yake kuna kushangaa, kujua vyema jambo ambalo ulikuwa hulijui na kuwa na kiu ya kujua kinachoendelea.

SALA: Ee Yesu tujalie neema tutambue mafundisho yako.