Januari 5, 2022; Jumatano: Baada Ya Epifania

SOMO 1: 1Yn. 4:11-18
Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasari katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 72:1-2, 10, 12-13
K: Mataifa yote ya dunia watakusujudia, Ee Bwana.

  1. Ee MUngu, mpe mfalme hukumu yako,
    Na mwana wa mfalme haki yako.
    Atawaamua watu wako kwa haki,
    Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
  2. Wafalme wa Tarshishi na visiwa
    Na walete kodi;
    Wafalme wa Sheba na Seba
    Na watoe vipawa. (K)
  3. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
    Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
    Atamhukumu aliye dhaifu na maskini,
    Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

INJILI: Mk. 6:45-52
Baada ya watu elfu tano kula na kushiba, mara Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, “Changamkeni; ni mimi, msiogope.” Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.

TAFAKARI;
DHIHIRISHO LA UPENDO NI UTULIVU/UPENDO WA KWELI HUFANYA MAAJABU: Kuku (mtetea) mwenye vifaranga huwa na tabia ya kuvikunyata vifaranga vyake ndani ya mabawa yake ili kuvipa joto na kuvilinda dhidi ya hatari na hivyo vinakuwa salama. Vinaweza hata kuwa vingi lakini sio rahisi kujua kwani namna anavyovikunyata ni utaalamu usioweza kuelezeka kirahisi. Hii inaonesha upendo wa dhati kwa vifaranga hivyo, vinakaa ndani yake. Mfano huu unanisukuma kuona maelezo yaliyoko katika soma la kwanaza yalingane na huu mfano, tunaalikwa tukae ndani ya Mungu ili tuonje pendo lake la kweli. Ni pendo la kweli la Kristo ndilo lililomsukuma kuwaonea huruma wafuasi wake na kuwasaidia katika ile dhoruba kama Injili inavyoeleza. Jamii ya leo mambo mengi hayaendi kutokana na upendo wa kweli kukosekana.

SALA: Ee Yesu tujalie tuonje pendo lako.