Januari 4, 2022; Jumanne: Baada Ya Epifania

Mt. Elizabeth Ann Seton

SOMO 1: 1 Yn. 4:7-10
Wapenzi, tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 72:1-4, 7-8
K: Mataifa yote ya dunia watakusujudia, Ee Bwana.

 1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
  Na mwana wa mfalme haki yako.
  Atawaamua watu wako kwa haki,
  Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
 2. Milima itawazalia watu amani,
  Na vilima navyo kwa haki.
  Atawahukumu walioonewa na watu,
  Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye muonea. (K)
 3. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
  Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
  Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
  Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)

INJILI: Mk. 6:34-44
Siku ile, Yesu aliona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, “Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula.” Akajibu, akawaambia, “Wapeni ninyi chakula.” Wakamwambia, “Je! twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula?” Akawaambia, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame.” Walipokwisha kujua wakasema, “Mitano na samaki wawili.” Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote. Wakala wote wakashiba. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia. Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume.

TAFAKARI:
UPENDO HULETA LADHA KATIKA JAMII: Neno upendo hutamkwa mara nyingi sana katika mazungumzo yetu na hata wakati mwingine ili kuonyesha msisitizo tunatumia lugha za kigeni “Love” ukweli ni kuwa kutamka upendo na kuuishi upendo ni vitu viwili tofauti, twaweza kuwa tunatamkiana neno upendo lakini hatuuishi upendo wenyewe, na ndio maana Yohana katika somo la kwanza anasema upendo wetu chanzo chake kiwe ni Mungu mwenyewe. Hata jamii ya mitume wakati wakiwa na Bwana wao (Yesu) kama injili isemavyo, Yesu aliwaonesha namna ya kuishi maisha ya upendo wa kweli ambapo ni pamoja na kujali na kutatua shida za wengine, kuwa na huruma. Upendo ukikosekana unaleta utengano, ona mitume walitaka Yesu awaage watu waondoke waende kwao, lakini Yesu anawaonya, ‘hapana wapeni ninyi chakula,’ onesheni upendo wenu kwao, tubaki pamoja. Upendo huleta umoja na mshikamano.

SALA: Baba tunaomba utumiminie upendo wako tuweze kupendana kindugu.