Januari 3, 2022; Jumatatu: Baada Ya Epifania

Jina Takatifu la Yesu
Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: 1Yn. 3: 22-24; 4:1-6
Wapenzi: Lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa. Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu; nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia. Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 2:7-8, 10-11
K: Nitakupa mataifa kuwa urithi wako.

 1. Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
  Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
  Uniombe, nam nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
  Na miisho yote ya dunia kuwa milki yako. (K)
 2. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
  Enyi waamuzi wa dunia mwadibiwe.
  Mtumikieni Bwana kwa kicho;
  Shangilieni kwa kutetemeka. (K)

INJILI: Mt. 4: 12-17, 23-25
Siku ile, Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya; akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia.” Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani.

TAFAKARI:
JINA LINAMDHIHIRISHA MHUSIKA: Leo Mama Kanisa anasherehekea Jina Takatifu la Yesu. Amri ya Pili ya Mungu inatukataza kutotaja bure Jina la Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa unapotaja Jina la Mungu kwa heshima na unyenyekevu ni njia mojawapo ya kuomba msaada wake. Hata katika jamii zetu, tunashuhudia baadhi ya ofisi, watu hawathubutu kutaja ovyo majina ya mabosi wao bila sababu ya msingi ili kuonesha heshima kwake. Ulimwengu wa leo kila uchwao tunashuhudia katika mitaa yetu madhehebu yakiibuka na watu wanataja hovyo hovyo jina la Yesu ili kuwavuta watu, inakuwa kama mzaha au mchezo wa kuigiza. Unakuta mtu anarudia zaidi ya mara 10 “kwa jina la Yesu” hadi inakuwa karaha. Huko ni kumkebehi Mungu. Watu tanayumba kiimani kutokana na kutaka zaidi ishara kubwa kubwa na ndio maana hata katika Injili tunaona wengi wanaandamana na Yesu baada ya kuona ishara za kuponywa. Hii wakati mwingine inakuwa ni imani ya muda mfupi, haidumu, mtu leo anasali hapa kesho kule, bendera fuata upepo.

Sala: Ee Yesu tujalie tuwe na heshima kwa Jina lako.