Januari 2, 2022; Jumapili: Epifania

SOMO 1: Isa. 60:1-6
Ondoka, ee Yerusalemu, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako. Inua macho yako, utazame pande zote; Wote wanakusanyana; wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali, Na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia. Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 72:1-2, 7-8, 10-13
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

 1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
  Na mwana wa mfalme haki yako.
  Atawaamua watu wako kwa haki,
  Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
 2. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
  Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma
  Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
  Toka mto hata miisho ya dunia. (K)
 3. Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi,
  Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
  Naam, wafalme wote na wamsujudie;
  Na mataifa yote wamtumikie. (K)
 4. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
  Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
  Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
  Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

SOMO 2: Efe. 3: 2-3, 5-6
Ndugu zangu: Ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho: ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

INJILI: Mt. 2 : 1-12
Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao: Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda, kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakaye wachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota, Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.

TAFAKARI:
MUNGU ANATUTAKA WOTE NYUMBANI MWAKE: Hakuna chochote alichoumba Mungu kilicho najisi, ndiyo kisa kila alichoumba kinasemwa kilikuwa kizuri sana (Mwa 1:17.21.25). Kama ndivyo, mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake ni zaidi (Mwa 1:26-28). Mwanadamu alimwaga mboga kwa kutotii pale bustanini Edeni, lakini kwa upande wake, Mungu hakutaka kumwaga ugali na kupindua meza. Ndipo aliporuhusu mradi wa kupatanishwa naye. Wanadamu walijaribu kujipatanisha kwa sadaka na kafara mbalimbali, zikiwemo za wanyama, vyakula na vinywaji (Ebr 10:5-7) pasipo kukidhi haja. Hatimaye, mwana wa Mungu Yesu Kristo akajitolea kuwakomboa watu. Kusudi apate mwili na damu vya kumtolea Mungu sadaka ya kupendeza na hatimaye aweze kufa msalabani kwa ajili yao, alijimwilisha (Yn 1:1-14, Gal 4:4-7).
Sherehe ya Epifania ni wasaa wa kufurahia kufunuliwa kwa mradi mkubwa wa Mungu kutukomboa watu wote. Epifania inamaanisha “kuonekana juu ya” ni kukumbuka na kuishi upya ukweli kwamba Mungu anajionyesha kwa watu wote kusudi anayetaka kujishirikisha katika mradi wa ukombozi wa wanadamu wote ajipatie uzima wa milele na asiyetaka kujishirikisha kikimpata chochote mwishoni mwa maisha haya, ajilaumu mwenyewe.
Mungu kujionesha kwa watu hakuishii katika sherehe ya leo tu bali kuna sura nyingine katika sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Yesu Kristo atakapotambulishwa mbele ya wadhambi waliokuwa wakifika kubatizwa kwa Yohane Mbatizaji na pia Yesu Kristo atakapojitambulisha kwa watu wenye furaha harusini Kana.

Sala: Ee Mungu tunakushukuru kwa nia na mpango wako wa kutukomboa, tupe mioyo laini tushirikiane nawe ili nia yako kwetu itimie. Amina.