Januari 1, 2022; Jumamosi: Maria Mtakatifu Mama Wa Mungu

Sherehe
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO I: Hes. 6:22-27
Bwana alinena na Musa, na kumwambia, “Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; ‘Bwana akubarikie, na kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani. Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 67:1-2, 4, 6-7

 1. Mungu na atufadhili na kutubariki,
  Na kutuangazia uso wake.
  Njia yake ijulike duniani,
  Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
  K: Mungu na atufadhili na kutubariki.
 2. Mataifa na washangilie,
  Naam, waimbe kwa furaha,
  Maana kwa haki utawahukumu watu,
  Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)
 3. Nchi imetoa mazao yake;
  Mungu, Mungu wetu, ametubariki.
  Mungu atatubariki sisi;
  Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)

SOMO 2: Gal.4:4-7
Ndugu zangu: ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.

INJILI: LK. 2:16-21
Siku ile: Wachungaji walienda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.

TAFAKARI:
MAMA WA MFALME MSAADA WA WATU: Kumbe, katika sherehe ya leo ya Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu tunawekewa bayana msaada muhimu. Katika nafasi hiyo ya umama, uwezo na nia ya kutusaidia sisi anayo. Umama wa Mungu wa Maria si kwa ajili ya fahari yake binafsi, isipokuwa unavuka hilo na kuwa msaada wa raia wa ufalme wa Mungu unaojengwa sasa. Ndiyo maana huwa tunasali katika Salamu Maria, “Maria mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu”. Kwa jinsi hii sala zote zinazomwomba Mama Bikira Maria atuunganishe na mwanawe zina nguvu za pekee na baraka nyingi: Salamu Maria, Memorale, rozari, Litania ya Bikira Maria na kadhalika zina nguvu sana ilmradi tunasali kwa imani. Kuupuuza sala kwa Mama Bikira Maria ni kama mtu kujaribu kufika mahali kwa haraka kwa kukimbia kwa miguu huku akiacha kupanda gari liendalo aendako.

SALA: Ee Mungu tufundishe kupunguza mahangaiko yetu kwa kupendelea kumwalika Bikira Maria Mama wa Mungu atuombee.