Mt.Silvestri I, Baba Mtakatifu
Nyeupe
Zaburi:Juma 1
SOMO 1: 1 Yoh 2:18-21
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu. Nanyi mmepakwa mafuta na yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli.
WIMBO WA KATIKATI Zab. 96, 1-2, 11-13
1.Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
2.Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
3.Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
INJILI: Yn 1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohane alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.
Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
TAFAKARI
LAZIMA KUMKIRI KRISTO KWA MANENO NA MATENDO: Leo ni mwisho wa mwaka. Kitabu cha Mhubiri 3:1-8 kinaeleza habari za majira na nyakati. Kila jambo lina wakati wake. Mtume Yohane anawaeleza Wakristo kuwa wasitegemee mambo yaende tu kwa ulaini. Anaelekeza kuwa pamoja na kumwamini Kristo watatokea wapinga Kristo na kuwa wapo pia kati yetu. Tunatakiwa kumkiri Kristo kwani kwa kufanya hivyo tunamkiri pia Baba na tunaendelea kukaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba. Zawadi ya kumkiri huko ni kupata uzima wa milele. Kwa tendo la umwilisho Neno wa Mungu amekubali kukaa nasi katika hali yetu ya kibinadamu Nasi tupokee upendeleo huo tumruhusu aendelee kukaa ndani yetu nasi ndani yake. Tunapomshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka tujihoji nafsini mwetu, imani yetu kwa Kristo ipo namna gani. Imani yetu inaturuhusu kusema tupo ndani ya Kristo na Baba au tupo nje. Kama tupo nje tuanze mwaka mpya na mikakati mipya ya kuwa ndani ya Kristo.
Sala: Ee Yesu, Bwana wa nyakati zote, tunaomba utujalie neema ya kuendelea kubaki ndani yako. Tujalie mwaka mpya wenye heri na baraka zako.