DESEMBA 30,2021 ALHAMISI: OKTAVA YA KUZALIWA BWANA

Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: 1 Yoh 2: 12-17
Nawaandikia ninyi watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake. Nawaandikia ninyi akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi watoto, kwa sababu mmemjua baba, Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmeshinda yule mwovu.
Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.

WIMBO WA KATIKATI :Zab 96:7-10

1.Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu,
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
2.Leteni sadaka mkaziingie nyua zake,
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu,
Tetemekeni mbele zake, nchi yote. (K)
3.Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam,ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)

INJILI:Lk 2: 36-40
Siku ile palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

TAFAKARI
NI WAJIBU WETU KUTIMIZA SHERIA YA BWANA: Katika utaratibu wa Kiyahudi mtoto wa kwanza wa kiume alipaswa kutolewa hekaluni. Walikuwa wanamtolea shekeli tano ili kuachwa huru asilazimike kuwa kuhani. Wazazi wake Yesu walitimiza sheria hiyo kwa uaminifu mkubwa. Ni katika uaminifu huo baada ya kumtolea mtoto hekaluni wanarudi Galilaya na mtoto Yesu. Kwa kuwa ameshakabidhiwa kwa Mungu anapata nguvu na amejaa hekima ya kimungu. Hekima hiyo imejionesha jinsi Yesu alivyokuwa akifanya kazi zake. Tunaalikwa kuiga mfano wa kuwakabidhi watoto kwa Mungu ili wapate nguvu na hekima. Tusiwakabidhi watoto kwa wanadamu wasio na nguvu aliyo nayo Mungu. Tunapowapeleka kubatizwa tusiwachanganye tena na mambo ya kidunia. Imani yetu kwa Mungu ibaki imara kama ya huyu mama mjane aliyeweza kushuhudia makuu ya Mungu. Mama huyu aliweza kutembea katika lile tulilosikia katika somo la kwanza kutokuupenda mno ulimwengu na mambo yake. Tusichuchumilie mno ya kiulimwengu bali tuchuchumilie yaliyo juu.

Sala: Ee Yesu mpenzi, nijalie niwe na hekima katika utendaji wangu wa kila siku