DESEMBA 28,2021 JUMANNE: OKTAVA YA KUZALIWA BWANA

WAT. WATOTO MASHAHIDI
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: 1Yoh. 1:5 – 2:2
Hii ndiyo habari tulioisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni Nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu. Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

WIMBO WA KATIKATI: Zab124:1-4, 7-8

1.Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia.
(K) Nafsi yetu imeokoka kama ndege,
katika mtego wa wawindaji.
2.Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu;
Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu; (K)
3.Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
Msaada wetu u katika jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi. (K)

INJILI: Mt 2:13-18
Mamajusi walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.

TAFAKARI
UCHU WA MADARAKA HUSABABISHA MADHARA MAKUBWA: Katika Injili tunapata habari za mahangaiko aliyokuwa nayo Herode akidhani kuwa mfalme aliyepata habari zake yaani Yesu, amekuja kuchukua ufalme wake. Aliamini kuwa kuzaliwa kwa Yesu madaraka yake yanaondoka kwani alikuwa na dasturi ya unyonyaji na kung’ang’ania madaraka. Uchu wa madaraka unamfanya awe na maamuzi mabaya ya kuwaua watoto wasio na hatia akiamini kuwa mauaji hayo yatafanikisha kifo cha mtoto Yesu. Tunaishi katika wakati ambao mambo hayako tofauti sana. Kuna mauaji ya mimba yanayofanyika kwa lengo la kukimbia majukumu, kubaki na sifa fulani na kadhalika. Si kitu kigeni kusikia watu wanauana kwa sababu ya madaraka na mali na hivyo wanashindwa kumwona Mungu aliye Mwanga na wanakumbatia dhambi. Mtume Yohane anatuhimiza tukiri na kuungama dhambi tupate kusamehewa. Tuwe wanyenyekevu wa kumpokea sakramenti ya huruma ya Mungu, ndiyo Kitubio.

Sala: Ee Mungu wangu, nijalie kuona thamani ya zawadi ya uhai wangu na wengine.