DESEMBA 27,2021 JUMATATU: OKTAVA YA KUZALIWA BWANA

MT.YOHANE, MTUME NA MWINJILI
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: 1Yoh 1:1-4
Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya neno la uzima; (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu); hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.

WIMBO WA KATIKATI :Zab 97: 1-2, 5-6, 11-12

1.Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.
2.Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake. (K)
3.Nuru imemzukia mwenye haki,
Na furaha wanyofu wa moyo.
Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana,
Na kulishukuru jina lake takatifu. (K)

INJILI: Yn 20:2-8
Siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena alikwenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza kufika kaburini, akaona na kuamini.

TAFAKARI
USHUHUDA KUHUSU UFUFUKO WA KRISTO: Somo letu la kwanza leo lina uhusiano wa karibu sana na Injili ya Yohane 1:14 naye Neno akawa mwanadamu akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake yeye aliye mwana wa pekee wa Baba, amejaa neema na ukweli. Wale walionshuhudia Neno wa Mungu (Kristo) ndio wanaohubiri walichoona, wakakijua na sasa wanamtangaza. Tangazo hili linasisitiza neno la uzima na tunaweza tu kufikia kwenye uzima kwa njia ya Neno. Neno huyu ndiye anayeshuhudiwa na yule mwanafunzi aliyempenda kuwa hayupo kaburini. Kadiri ya ufunuo wa Mungu mwanafunzi huyu ni Yohane ambaye amekuwa mfuasi mwaminifu wa Yesu tangu mwanzo wa utume wake, kazi zake, mateso yake na hata kifo na ufufuko wake. Tunapata mwaliko wa Mungu wa kujitahidi kumshuhudia Kristo kwa maisha yetu ya kila siku kama Yohane alivyofanya. Kumshuhudia Kristo kunahitaji sadaka kubwa, hivyo tuombe neema ya kuwa majasiri wa kushuhudia imani yetu mpaka mwisho bila hofu.

Sala: Ee Yesu naomba maneno na matendo yangu yakushuhudie daima.