DESEMBA 26,2021 DOMINIKA:OKTAVA YA KUZALIWA BWANA

FAMILIA TAKATIFU
Sikukuu
Mwaka C
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: YbS 3:2-6, 12-14
Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana, na kutithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu baba yake atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake huweka akiba iliyo azizi. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukudhibitisha.

WIMBO WA KATIKATI Zab 128:1-5

1.Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia zake
Taabu ya mikono yake hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia zake.
2.Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako. (K)
3.Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana,
Bwana akakubariki toka Sioni.
Uone uheri wa Yerusalemu.
Siku zote za maisha yako. (K)

SOMO 2: Kol 3:12-21
Ndugu zangu, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

SHANGILIO Kol 3:15, 16
Aleluya, aleluya,
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu,
Aleluya.

INJILI: Lk 2:41-52
Wazee wake Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhni ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu

TAFAKARI
FAHAMU MAADUI WA FAMILIA: Sherehe hii ilianzishwa na Papa Leo XIII mwaka 1893. Papa Leo alianzisha sherehe hii baada ya kusikitishwa na kuvunjika kwa familia nyingi. Ubinafsi, uasherati na kutojali mafundisho ya ndoa takatifu ulisambaratisha familia nyingi za Ulaya. Watoto wengi walitelekezwa bila matunzo na kuwa ombaomba mitaani. Papa Leo alitaka kuonesha kwamba maisha yetu ya familia yaige familia ya Nazareti. Familia ya Nazareti iliishi maisha ya kawaida bila kutengana. Ilikumbana na maadui kama umaskini na wivu lakini haikusambaratika. Yosefu alifanya kazi kwa bidii kumlisha mtoto wake. Wazazi wa Yesu walijitahidi kumtunza mtoto wao; hakutelekezwa na kuachwa kuzurura mitaani (Lk 2:41-52). Wapo wazazi wengi ndani ya familia walioendekeza uzembe na kuwafanya watoto wao waishi katika mateso. Tunaalikwa kuiiga familia hii takatifu. Kila mmoja wetu aangalie ni namna gani maisha ya familia hii yanapata ukamilifu ndani ya maisha yake.
Wimbo wetu wa katikati unatoka Zaburi ya 128. Ni zaburi ya familia. Inasisitiza kwamba ili familia iweze kubarikiwa lazima imche Mwenyezi Mungu. Ndipo familia itachanua na kuona amani. Kumcha Mungu ni kwa faida kubwa. Somo la kwanza linaelezea faida iliyopo kwa mtoto kumheshimu baba yake. Heshima kwa wazazi huleta faida kubwa. Yafaa mtoto abembeleze baraka hizi toka kwa wazazi wake. Anayesahau kuomba baraka toka kwa wazazi wake huyadhuru maisha yake.
Injili yetu ya leo inatueleza kwamba familia takatifu iliishi maisha ya kawaida. Ilikumbana na shida mbalimbali na kukabiliana nazo. Iliishi kwa kipato cha kawaida. Pia walikumbana na watu wenye chuki waliokataa kuwapokea (Lk 2:7). Herode alitaka kumwangamiza mtoto wa familia hii. Lakini yafaa tujiulize swali hili: Ni nini kilichoisaidia familia hii? Sababu ya kwanza ni kwamba walimthamini mtoto wao zaidi ya yote. Walipomkosa ndani ya familia yao, walikwenda kumtafuta. Mtoto Yesu alikuwa moyo na matumaini ya familia hii. Alipokosekana ndani ya familia, walikuwa tayari kuacha kila kitu kumtafuta. Sisi nasi tunapaswa kuiiga familia hii. Tusikubali Yesu atupotee. Akipotea, tukamtafute, tumuulize ameenda wapi? Ukija nyumbani ukikuta hakuna Yesu shinda siku tatu hata zaidi ukimtafuta kama walivyofanya Yosefu na Maria. Familia ilikosa amani alipokosekana mtoto. Yafaa tutambue kwamba amani ndani ya familia zetu haitapatikana ikiwa Yesu atakosekana.
Pia tunapaswa kuisikiliza sauti ya Mungu. Familia ya Nazareth haikuruhusu maneno ya nje kuwatenganisha. Kama Yosefu angalisikiliza umbea toka kwa majirani zake na kuitupa sauti ya Mungu, hakika angaliigawa familia yake. Yosefu aliruhusu malaika kuzungumza naye. Nyakati zetu malaika wanaongea na sisi bado lakini tunasikiliza ujumbe toka vijiweni kuliko ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu. Lazima tujifunze kukaa chini, na kusikiliza sauti ya malaika anayesema nasi ndani ya dhamiri zetu kama ilivyotokea kwa Yosefu (Mt 1:18-25).
Familia ya Nazareti ilisaidiwa na fadhili ya uvumilivu. Maisha yanahitaji uvumilivu. Kwenye kuwalea watoto, tunahitaji uvumilivu mkubwa, wanandoa wanahitaji uvumilivu mkubwa. Wanafamilia wasiisahau fadhila hii ndani ya familia zao. Hakika hili ni jambo la muhimu sana. Familia ya Nazareth ilisaidiwa na fadhila ya umoja. Kinachozisambaratisha familia nyingi ni kutokukaa pamoja hasa baadhi wanapofanikiwa. Wapo ambao baada ya mafanikio, huchagua marafiki wengine na kuwatelekeza wanafamilia yao. Tuzipinge tabia za namna hii. Tuzipende familia zetu. Tabia ya kutafuta marafiki na kuwatenga wanafamilia ni ubinafsi mkubwa.
Vilevile katika familia zetu, watoto wapatiwe kipaumbele cha pekee. Mali za familia zitumike kwa ajili yao na si kutapanywa katika uasherati na ulevi. Wapo watoto wanaokosa kusoma kwa sababu ya matumizi mabaya ya mali za familia. Wapo waliotelekezwa na baadhi kupata utapiamlo kutokana na uzembe wa wazazi. Yafaa kupingana na tabia za namna hii. Wapo pia baadhi ya wanafamilia wenye tabia za udokozi. Hawa hudokoa mali za familia kwa maslahi binafsi. Wapo wanafamilia wenye kuzirudisha nyuma familia zetu kwa kuiba vifaa vya kilimo kama majembe na mashine mbalimbali. Wapo tayari kufurahishwa na kilevi kuliko maendeleo ya familia. Yafaa tuache tabia za namna hii.

Sala: Ee Bwana, nisaidie mimi kuishi kama katika familia takatifu, tukiungana sote katika kuheshimiana kwa upendo.