DESEMBA 24,2021 IJUMAA: JUMA LA 4 LA MWAKA

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: 2 Sam 7:1-5, 8-11, 16
Ikawa, mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe.
Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, enenda, ukamwambie mtumishi wangu Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibibishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

WIMBO WA KATIKATI Zab 89:1-4, 27, 29

1.Fadhili za bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote
Uaminifu wako.
Maana nimesema, fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
2.Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele;
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)
3.Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza;
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
Wazao wake nao watawadumisha milele,
Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu. (K)

INJILI: Lk 1:67-79
Siku ile, Zakaria, baba yake Yohane alijazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,
Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; tuokolewe na adui zetu na mikononi mwao wote wanaotuchukia; ili kuwatendea rehema baba zetu, na kulikumbuka agano lake takatifu; uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, ya kwamba atatujalia sisi, tuokoke mikononi mwa adui zetu, na kumwabudu pasipo hofu, kwa utakatifu na kwa haki mbele zake siku zetu zote.
Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.

TAFAKARI
KUJENGA NYUMBA YA MUNGU: Katika somo la kwanza tumeona tamanio la mfalme Daudi kumjengea Mungu nyumba (2 Sam 7:2). Mawazo ya Mungu yanakuwa tofauti na mawazo ya Daudi. Mwenyezi Mungu anaahidi kuwa yeye ndiye atakayemjengea Daudi nyumba (2 Sam 7:11). Ahadi ya Mwenyezi Mungu inatimia katika katika unabii anaoutoa Zakaria “Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake” (Lk 1:69). Yohane ndiye anayetayarishwa kumtengenezea Bwana njia kwa kuwajulisha watu wokovu kwa maondoleo ya dhambi zao ili watoke katika uvuli wa mauti. Neno hili la Mungu litukumbushe kuwa matamanio yetu ya kuwa karibu na Mungu Mwenyezi ni jambo jema na Mungu hubariki matamanio hayo hata kama hatupati jibu la haraka kwa akili zetu za kibinadamu kwani Mungu hutimiza viapo vyake. Sisi tangu ubatizo wetu kuna viapo tulivyomwapia Mungu kwa kukiri imani na kukataa kuongozwa na Ibilisi. Tutimize viapo vyetu tuishi kwa uaminifu kusudi tuendelee kuwa karibu na Mungu.

Sala: Ee Mungu Mwenyezi, naomba nijalie kudumu mwaminifu kwa ahadi zangu za ubatizo.