DESEMBA 23,2021 ALHAMISI: JUMA LA 4 LA MAJILIO

Mt.Yohane wa Kanti, Padre
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mal 3:1-4, 5-6
Bwana Mungu asema: angalieni namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani. Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo wa watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.

WIMBO WA KATIKATI:Zab 25:4-5,8-10,14

1.Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako.
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.
(K) Changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu,
kwa kuwa ukombozi wenu unakaribia.
2.Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
3.Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao,
Naye atawajulisha agano lake. (K)

INJILI:Lk 1:57-66
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elizabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema, La, sivyo; bali ataitwa Yohane. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hili. Wakamwashiria babaye wajua atakavyo kumwita. Akataka kibao akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohane. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

TAFAKARI
TUANDAE NJIA YA BWANA: Katika neno la Mungu leo, Mwenyezi Mungu anaahidi kwamba atamtuma mjumbe wa kuandaa njia kwa ajili ya kuja kwake mwenyewe kutoa hukumu na kutangaza agano lake. Mjumbe huyu atakuwa na kazi ya kuondoa yale yaliyo kinyume na maagizo ya Mungu. Katika Injili mjumbe huyu anaonekana kuwa ni Yohane Mbatizaji ambaye watu waliokuwa karibu na wazazi wake waliingiwa na hofu wakawa wanajiuliza mioyoni mwao mtoto huyo atakuwa wa namna gani. Tunapokaribia kusherekea Noeli tujiandae vema kiroho kwa kutubu dhambi zetu mbele ya Mungu Mwenyezi na mbele ya wenzetu na kujipatanisha nao. Tutengeneze njia ya Bwana kwa kuondoa vizuizi tulivyojiwekea ili tuweze kujipatanisha na Mungu. Tufungue kufuli za mioyo yetu ili Masiha aweze kuingia ndani yetu na kutenda kazi ndani yetu. Masiha anayekuja ni zawadi kutoka kwa Mungu na tunatakiwa kuipokea katika hali ya neema ya utakaso.

Sala: Ee Yesu mwema, naomba unisaidie kujiachanisha na yale yasiyomtukuza Mungu.