DESEMBA 22,2021 JUMATANO: JUMA LA 4 LA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: 1 Sam 1:24-28
Siku zile, Hana alimchukua Samweli pamoja naye, na ng’ome watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa Bwana, huko Shilo; na yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. Nao wakamchinja huyo ng’ombe, wakamleta mtoto wa Eli. Hana akasema, Ee Bwana wangu, kama iishivyo roho yako, Bwana wangu, mimi ni yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana. Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.

WIMBO WA KATIKATI 1Sam. 2:1, 4-8

1.Moyo wangu wamshangilia Bwana,
Pembe yangu imetukuka katika Bwana.
Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu;
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
(K)Moyo wangu wamshangilia Bwana mwokozi wangu.
2.Pinde zao mashujaa zimevunjika,
Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
Ha hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. (K)
3.Bwana huua, naye hufanya watu hai;
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufurahisha mtu, naye hutajirisha;
Hushusha chini, tena huinua juu. (K)
4.Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakarithi kiti cha enzi cha utukufu. (K)

INJILI: Lk 1: 46-56
Siku ile Maria alisema: Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa; kwa kuwa mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; ili kukumbuka rehema zake; kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

TAFAKARI
KUSHUKURU NI JAMBO JEMA. Masomo yote mawili yanaelezea shukrani ya viumbe kwa Mwenyezi Mungu. Shukrani hii ni tofauti kabisa na mawazo ya kawaida ya wanadamu ambayo ni kusikia sauti ya kusifiwa. Hana alisali akimwomba Mungu apate mtoto na akatoa ahadi kwa Mungu. Katika somo la kwanza leo tunapata habari za sadaka ya shukrani ya Hana kwa Mwenyezi Mungu. Aidha Mama Bikira Maria anatoa sala yake ya shukrani kwa Mungu (Magnificat) ikiwa na maudhui mengi ya furaha, shukrani, masifu ukunjufu wa moyo unyenyekevu na utii kwa Mungu. Hana pamoja na Mama Bikira Maria wanatualika kurejesha sifa zote kwa Mungu na siyo kupenda kusikia tukisifiwa tu. Masomo yetu yanatufundisha pia tuwe watu wa kushukuru kwa makuu anayotuendea Mungu. Mara kadhaa huwa tunasikia watu wakiomba Misa kwa nia ya ombi fulani. Baadhi hurudi kushukru baada ya kupata hitaji lao wengine hutokomea kabisa Basi tunapoomba tuwe tayari kushukuru tunapofanikiwa.

Sala:Ee Mungu Baba, naomba unijalie moyo wa kushukuru kwa kila jambo.