Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Isa 7:10-14
Siku zile, Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
WIMBO WA KATIKATI:Zab 24: 1-6
1.Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yane juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Mfalme wa utukufu apate kuingia.
2.Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
3.Atapokea baraka kwa Bwana,
Ila haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, ee Mungu wa Yakobo. (K)
INJILI: Lk 1: 26-38
Malaika Gabriel alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni MariAmu
Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?
Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elizabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
TAFAKARI
NAFASI YA BIKIRA MARIA KATIKA UKOMBOZI WETU: Wapendwa familia ya Mungu katika Injili ya leo tunaona nafasi ya Mama Bikira Maria katika mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu Unyenyekevu wa Mama Bikra Maria umekuwa msaada mkubwa kwetu kumpata Mkombozi kwani ni katika unyenyekevu huo amekubali mpango wa Mungu utendeke ndani yake. Ahazi tuliyemsikia katika somo la kwanza alisita kupokea ujumbe wa Mungu lakini Mama Maria aliupokea kwa unyenyekevu. Mama Maria alipata zawadi ya kuwa tabernakulo ya kwanza ya kumbeba Yesu. Hii ni kwa sababu ya usafi wa moyo na unyenyekevu wake. Alikuwa tayari kutoa sadaka mipango yake ya awali ili kupokea kwanza mpango wa Mungu. Nasi Mungu anapotutaka kwa jambo fulani la kujenga Kanisa lake tusiwe na visingizio bali tumpe nafasi ya kwanza kabisa na hayo mengine yatafuata. Unyenyekevu wa Mama Bikira Maria umemnyanyua na kumkweza juu kabisa Tumwombe mama huyu atuombee fadhila ya unyenyekevu.
Sala: Ee Yesu naomba uniongezee fadhila ya unyenyekevu.