DESEMBA 19,2021 DOMINIKA: DOMINIKA YA 4 YA MAJILIO

Mwaka B
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mik 5:2-4
Bwana asema: wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia. Na mtu huyu atakuwa amani yetu.

WIMBO WA KATIKATI Zab 80:1-2, 14-15, 17-18

1.Wewe uchungaye Israeli usikie,
Wewe uketie juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nguvu zako.
Uje, utuokoe.
(K) Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
2.Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda
Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya
Kuwa imara kwa nafsi yako. (K)
3.Mkono wako na uwe juu yake
Mtu wa mkono wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya
Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. (K)

SOMO 2: Ebr 10:5-10
Ndugu zangu: Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, Kristo asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

SHANGILIO Lk 1:38
Aleluya, aleluya,
Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana;
na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Aleluya.

INJILI: Lk 1:39-45
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti. Ikawa Elizabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.

TAFAKARI
FUNGUKA, JIANDAE KUZIPOKEA BARAKA ZA MWENYEZI MUNGU:
“Dondokeni enyi mbingu toka juu na mawingu yamwage mwenye haki.” Haya ni maneno toka Isaya 45:8. Ni unabii uliotolewa na Isaya wakati wana wa Israeli wakiwa utumwani Babiloni. Kitendo cha wao kuwa utumwani kiliashiria ukosefu wa haki, kwamba dunia haina haki. Walidiriki kuamini kwamba ulimwenguni, wapo wanaopaswa kutawala na wengine wa kufanywa watumwa nabii Isaya anatangaza kwamba Mwenye Haki atatokea. Huyu Mwenye Haki walitamani atoke mbinguni, amwagwe kama mawingu toka juu kwani waliona kwamba Mwenye Haki hawezi kutokea duniani. Walitamani mbingu kufunguka na kummwaga Mwenye Haki.
Katika somo la kwanza, nabii Mika anaelezea tabia za huyu mfalme Mwenye Haki. Yeye kwa kipindi chake, amani na haki vitatawala. Ataongoza kwa nguvu ya mkono wa Mungu na kipindi chake watu wote watakuwa salama. Haya yote yametimia kwa ujio wa Yesu. Yesu aliwapenda wote na kutamani wabakie salama. Alijitoa ili wengine wafaidi. Alikubali hata kufa msalabani ili wengine wapone.
Kwenye haya masomo yetu twajifunza mambo makuu mawili. Kwanza, haya yalikuwa ni maneno matakatifu, ya Mungu anayeamuru baraka ziwamwagikie watu wake. Anawaeleza watu wake wazipokee na kutembea kati yake. Nchi inaambiwa sasa ifunguke, ijiandae kupokea baraka hizi. baraka hizi zinategemea jinsi nchi itakavyojifunua. Ikikataa kujifunua, itajifungia baraka hizi. Wote waliompokea Kristo walipokea uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu (Yn 1:12). Sisi tushirikiane na Bwana Yesu hasa katika sakramenti zake mbalimbali. Yafaa tufungue mioyo yetu na kuonja furaha ya kuwa na Bwana Yesu hasa kwa njia ya sakramenti zake.
Pili, tunahitaji wanadamu hasa viongozi wenye tabia kama za mfalme huyu atayamwagwa toka mbinguni. Viongozi wenye tabia za kujitolea kwa ajili ya wengine. Tunahitaji wazazi wenye kujitolea ili kuwafanya watoto wao waishi maisha mema na amani. Ili tuweze kufikia hili, yafaa tuwe watu wenye juhudi. Yesu alipokuwa na wanafunzi wake, alihakikisha kwamba wanaishi kwa amani. Viongozi wetu tujifunze kuiga tabia hizi.
Tatu, tumeona kwamba kiongozi huyu atafanikiwa kwa sababu ataongoza kwa nguvu na msaada wa Mungu. Sisi tujifunze kuomba msaada wa Mungu. Tunahitaji viongozi wa namna hii. Viongozi wasiomcha Mungu husababisha madhara makubwa ndani ya jamii. Tumtangulize Bwana mbele na hakika tutadumisha amani ndani ya jamii yetu. Kiongozi anayesafiri na Bwana hufaulu katika mengi. Tusimweke Bwana pembeni.
Katika Injili, Mama Maria anakwenda kumtembelea Elizabeti. Safari hii inakuwa sababu ya furaha kwa Elisabethi na na Yohane Mbatizaji aliyekuwa tumboni mwa Elizabeti. Maria aliweza kuleta furaha kwa hawa wawili kwa sababu ndani ya tumbo lake alimbeba Yesu, aliye asili ya furaha yote. Sisi tukazane kumfanya Yesu aje kati yetu. Hili itatufanya kuwa vyombo vya amani na furaha.
Yafaa tuelewe kwamba ni kwa njia ya sala tutaweza kupeleka ujumbe wa matumaini kwa wenzetu. Ukiwa na Bwana, utapeleka Habari Njema kwa mwenzako. Yafaa tujichunguze; mara nyingi tumeshindwa kuwa matumaini kwa jamii kwa sababu tunapeleka hasira na fujo kwa wenzetu. Tukimtegemea Mungu, hakika tutaweza kupeleka Habari Njema kwa wenzetu. Hata tunapotaka kwenda kuwashauri wenzetu, yafaa tuombe msaada toka kwa Mungu ili Bwana apate kuingia ndani yetu na hivyo tuweze kuwashauri wenzetu vyema. Mara nyingi tunashindwa kusuluhisha kesi za wenzetu kwa sababu ya kumkosa Roho wa Bwana ndani ya mioyo yetu.
Umuhimu wa Mama Maria kwa maisha ya Mkristo unaonekana tena katika Injili yetu leo. Elizabeti aliposogea karibu na Mama Maria, aliweza kuwa karibu zaidi na Yesu. Hili liwe fundisho na kwetu sisi Wakristo. Tutambue kwamba pale tunapokubali kusogea karibu ya Mama Maria, ndipo tutakapoweza kusogea karibu zaidi na Yesu na kufurahi kama ilivyotokea kwa Elizabeti. Tutamfikia Yesu kupitia kwa mama Maria. Tusiache kuwa karibu na mama kila wakati.

Sala: Bwana, ninaomba maisha yako ulioishi ya kibinadamu yawe msingi wa maisha yangu.