DESEMBA 18,JUMAMOSI: JUMA LA 3 LA MAJILIO

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO I: Yer 23:5-8
Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu. Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri; lakini, Aishivyo Bwana, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.

WIMBO WA KATIKATI:Zab 72: 1-2, 12-13, 18-19

1.Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
Na wingi wa amani milele.
2.Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na masikini,
Na nafasi za wahitaji ataziokoa. (K)
3.Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
Atendaye miujiza yeye peke yake;
Jina lake tukufu na lihimidiwe milele;
Dunia yote na ijae utukufu wake.
Amina na Amina. (K)

INJILI: Mt 1:18-24
Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

TAFAKARI
HAKI NA HURUMA KATIKA MAISHA YETU: Nabii Isaya anatangaza ujio wa utawala wa kimasiha. Katika utawala huo wa kimasiha, Isaraeli atafurahia haki na amani chini ya viongozi ambao ni chaguo la Mungu. Katika Injili tumemsikia pia Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki, akitenda haki kwa mchumba wake Maria. Alipomwona ni mjamzito alipata shaka kuhusu hali hiyo na kwa vile hakutambua kuwa ulikuwa mpango wa Mungu alikusudia kumwacha kwa siri kwani angemtangaza Maria angepigwa mawe mpaka kufa. Tujifunze kuwa watu wa haki kama alivyokuwa Yosefu kwa Maria. Haki inapokosekana kunakuwa na unyanyasaji, uonevu, vita na kadhalika. Tuwe watu wa haki kwanza kwa Mungu, kwa wenzetu na tujitendee haki sisi wenyewe. Pia tuwe watu wa haki kwa taifa letu na taifa litende haki kwa wananchi kwa kugawanya vema rasilimali za taifa. Tutende haki katika mazungumzo yetu, tutende haki kwa waajiri wetu na wahudumu au wafanyakazi wetu.

Sala: Ee Mungu Mwenyezi, Muumba mbingu na nchi, naomba unifanye chombo cha kutenda haki daima.