DESEMBA 17,2021 IJUMAA: JUMA LA 3 LA MAJILIO

SOMO 1: Mwa 49:2, 8-10
Siku ile, Yakobo aliwaita wanawe, akawaambia: kusanyikeni, msikie enyi wana wa Yakobo, msikilizeni Israeli, baba yenu. Yuda, ndugu zako watakusifu, mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni mwana-simba, kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; aliinama akajilaza kama simba, na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria katika miungu yake, hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.

WIMBO WA KATIKATI Zab 72:1-4, 7-8, 17

1.Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako
Na mwana wa mfalme haki yako
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
Na wingi wa amani milele.
2.Milima itawazalia watu amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa na watu,
Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea. (K)
3.Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)
4.Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling’aapo jua, jina lake liwe na wazao.
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
Na kumwita heri. (K)

INJILI: Mt 1:1-17

Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.
Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi.
Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babiloni.
Na baada ya ule uhamisho wa Babiloni, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zarubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliyakimu; Eliyakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo.
Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.
Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babiloni ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babiloni hata Kristo ni vizazi kumi na vinne.

TAFAKARI
SISI NI NDUGU KATIKA UKOO WA YESU: Katika somo la kwanza tumemsikia Yakobo kabla ya kufa kwake akitoa maelekezo au hatima ya maisha ya wanawe kwa maisha ya baadaye. Yakobo anamtabiria Yuda mambo makubwa na kuwa atakuwa na mafanikio tele juu ya ndugu zake na maadui zake watashindwa. Anamwahidi mamlaka na utawala mpaka Masiha atakaopokuja. Yawezekana hii ni kwa sababu ya utii na upendo aliokuwa nao kwa baba yake. Utabiri huu unakamilika katika katika Injili tunaposikia historia ya ukoo wa Yesu Kristo tangu Ibrahimu. Sisi ambao ni wabatizwa tunaingizwa katika ukoo wa Yesu kwa njia ya ubatizo wetu na hivyo tunaitwa Wakristo. Kwetu sisi Waafrika ukoo wa mtu ni wa muhimu sana na unathaminiwa kwa namna ya pekee. Watu wanaona fahari kwa koo zao. Sisi kama ukoo mteule wa Kristou tujionee fahari kwa ukoo wetu wa Kristo. Mtu akifanya kosa la kumtenganisha na ukoo wake hutaabika sana. Tusikubali kutengana na ukoo wetu wa Kristo kwa njia ya dhambi.

Sala: Ee Mungu Mwenyezi, naomba neema ya kutambua thamani ya ukoo wangu wa Kristo.